NJOMBE: Makamu wa Rais Dk Philip Isdori Mpango ametembelea Banda la Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Njombe wakati wa hafla ya kufunga Maonesho ya Nne ya Sido yanayoadhimishwa kitaifa mkoani humo.
Dk Mpango alitembelea Banda hilo Oktoba 28, 2023 alipokwenda kufunga Maonesho hayo yaliyoanza Oktoba 23, 2023 katika viwanja vya Sabasaba mkoani Njombe.
Akiwa katika Banda la Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Njombe, Makamu wa Rais alielezwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geofrey Pinda namna wizara ya Ardhi inavyotekeleza majukumu kwenye Mkoa wa Njombe ikiwemo zoezi la umilikishaji ardhi.
“Ofisi yetu ya Kamisha hapa Njombe imekuwa ilifanya kazi kubwa ikiwemo kuandaa hati miliki za ardhi na hapa kuna takriban hati 167 ambazo wamiliki wake hawajakuja kuzichukua” alisema Pinda.
Akielezea ushiriki wa ofisi yake katika maonesho hayo, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Njombe Fulgence Kanuti amesema, tangu kuanza kwa maonesho hayo Oktoba 23, 2023 ofisi yake imeweza kuandaa hati milki za papo hapo 18 na wahusika wamewwza kuzichukua.
Hata hivyo, amesema hati 167 ambazo wamiliki wake hawajazichukua ni za halmashauri ya Mji wa Njombe na ofisi yake inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wamiliki hao wanazichukua.
“Muitikio wa uchukuaji hati milki za ardhi hapa Njombe siyo mzuri sana, sababu naweza kusema watu hapa wako busy ila wanakuja kuchukua pale panapokuwa na uhitaji maalum kama vile mtu akihitaji mkopo benki”. Alisema Kanuti.
Hata hivyo, alisema baadhi ya juhudi zinazofanywa na ofisi yake katika kuhakikisha wananchi wa Njombe wanachukua hati ni kutoa matangazo ikiwemo kutumia redio jamii kuhamasisha.