Dk Mwinyi aagiza mabalozi fursa za uchumi
RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewataka mabalozi walioteuliwa hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Zimbabwe, Zambia na Uholanzi, kuitangaza Tanzania na kuona fursa za kiuchumi.
Dk Mwinyi alitoa mwito huo Ikulu Zanzibar alipozungumza na mabalozi hao watatu; Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro (Zimbabwe), Mathew Mkingule (Zambia) na Caroline Chipeta (Uholanzi).
Alisema kuna umuhimu kwa mabalozi hao kuitangaza vyema Tanzania katika nchi hizo kwa kuendeleza ushirikiano uliopo na kuangalia fursa za kiuchumi.
Dk Mwinyi alisema katika kutekeleza diplomasia ya uchumi, serikali imeweka kipaumbele sekta za uchumi wa buluu kwa lengo la kukuza uchumi.
Alimuagiza Balozi Chipeta kuweka nguvu ili kuongeza idadi ya watalii wa nchi hiyo wanaozuru Tanzania.
Aidha, aliwataka mabalozi hao kuchangamkia fursa za masoko ya mazao ya karafuu na viungo kwa kuwaunganisha wafanyabiashara wa nchi hizo na wa Zanzibar.
Aliwaagiza mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Zimbabwe na Zambia kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kwa kuangalia fursa za kibiashara na kuzingatia suala la ulinzi na usalama.