Dk Mwinyi aagiza ulinzi vyanzo vya maji

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameziagiza taasisi zinazosimamia masuala ya maji safi na salama ikiwamo Wizara ya Maji, Nishati na Madini na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), kulinda vyanzo vya maji na kuepusha ujenzi holela wa makazi ya kudumu.

Dk Mwinyi alisema hayo jana Unguja wakati akifungua kongamano la kimataifa la utafiti wa maji safi na salama. Alisema kuna matukio mengi ya ujenzi wa nyumba za kudumu na ukataji wa miti jirani na vyanzo vya maji hivyo juhudi na tahadhari vinahitajika kukabili tishio la kukauka kwa vyanzo hivyo.

Aidha, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema imejipanga kufanya kazi na watafiti na taasisi zilizobobea katika sekta ya maji ili Zanzibar ijitosheleze maji safi na salama.

Dk Mwinyi alisema maji ni uhai na ndiyo msingi wa maendeleo yote ikiwamo ukuaji wa uchumi na tafiti zinaonesha dunia itakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa maji safi na salama kutokana na kuwepo kwa changamoto mbalimbali kama mabadiliko ya tabianchi na ukame.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaibu Hassan Kaduwara alisema maji ni miongoni mwa vipaumbele vya SMZ kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo ya uhakika.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Joseph Kilangi alisema wameanza kufanya tafiti kuhusu upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa ikiwamo Norway, Shirika la Kimataifa la Global Partnership na Shirika la Kimataifa la Ujerumani katika maeneo ya utafiti wa maji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Global Partnership, Victor Konga alisema taasisi hiyo imesaini makubaliano na SMZ kufanya utafiti kuelewa kiwango cha maji na vyanzo vyake.

“Tumeanza kufanya utafiti kuhusu hali ya kiwango cha maji na upatikanaji wake pamoja na kuangalia vyanzo vinavyozalisha maji safi na salama,” alisema Konga.

Habari Zifananazo

Back to top button