Dk Mwinyi aita watalii, wawekezaji wa Qatar

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametoa mwito kwa Kampuni ya Abu Issa Holding ya Qatar kuangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya watalii Zanzibar. Dk Mwinyi amesema hayo alipokutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Kampuni ya Abu Issa Holding, Ashraf Abu Issa mjini Doha nchini Qatar.

Kampuni hiyo inajihusisha na uwakala wa usafirishaji watalii. Pia ameiomba ishawishi wawekezaji wengine waende kuwekeza katika visiwa vidogo vidogo vilivyopo Zanzibar. Dk Mwinyi pia amekutana na viongozi wa Kampuni ya Power International Holding.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wameonesha kupendezwa na mradi wa umeme wa Zanzibar, kuashiria fursa kubwa za uwekezaji katika sekta hii muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar.

Advertisement

Katika hatua nyingine, mke wa Rais Mwinyi, Mama Mariam Mwinyi amewasihi Watanzania wanawake wanaoishi Qatar waendeleze utaratibu wao wa kupeleka mchango na shukrani nyumbani na wasaidie wanawake Zanzibar.

Mama Mariam ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora alisema hayo alipohutubia wana-diaspora wanawake walioko Qatar wakati wa sherehe za kutimiza mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa taasisi yake.

Alitoa mwito kwa wanawake hasa wana-diaspora waishio Qatar wawe makini katika malezi ya watoto ili kukabili vitendo vya udhalilishaji. Alihimiza akina mama wawe mstari wa mbele kuchukua hatua za mapema kuzuia udhalilishaji wanawake wajenge mazingira salama ili watoto wapate malezi bora.

Jana Dk Mwinyi alitarajiwa kushiriki katika sherehe za ufunguzi wa Jukwaa la Kimataifa la Tatu la uchumi jijini Doha. Dk Mwinyi anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika jukwaa hilo.