ZANZIBAR: Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amesema amefarijika kwa Jumuiya ya Veteran Young Pioneers Zanzibar kumpongeza kwa kutekeleza vizuri ilani ya uchaguzi ya CCM katika kipindi cha miaka mitatu kwa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Rais Dk Mwinyi amesema hayo alipokutana na maveterani hao wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Khamis Rajab Mnubi Ikulu Zanzibar Februari 28, 2024.
Aidha Rais Dk Mwinyi amesema ataongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kutekeleza ahadi zote alizowaahidi wananchi wa Zanzibar.
Vilevile, Rais Dk Mwinyi ameipongeza Jumuiya hiyo kwa kuendeleza majukumu ya kujitolea kuwafundisha vijana uzalendo, ukakamavu na itikadi ya chama.
Jumuiya ya Veteran Young Pioneers ilianzishwa rasmi Desemba 20, 2015 chini ya sheria No:6 ya 1995 kwa kujumuisha wanachama ambao wametokana na Umoja wa Young Pioneers ulioasisiwa Machi 01,1964 mara baada ya Mapinduzi Matukufu.