RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi ameendelea kuhimiza wawekezaji wa China kuangalia fursa zilizopo za kuwekeza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Ameyasema hayo leo alipokutana na wawekezaji na wenye kampuni mbalimbali za hapa China.
Mapema asubuhi alikutana na Kampuni kubwa za kiufundi za KVS Chemical, Hunan Communications, Economic Engineering, Afri Greencrops Group na Sino Tech Kibaha Industrial Park.
Katika mazungumzo yao Rais Dk. Mwinyi amesisitiza ushirikiano wa China na Tanzania ni wa kihistoria na wawekezaji hao amewaambia sera kuu na muhimu ya Zanzibar ya uchumi wa buluu, ambapo vipengele vinne vilivyomo waangalie namna fursa zitakazowafaa wazichangamkie.
Amewafahamisha chini ya mwamvuli wa sera ya uchumi wa buluu kuna utalii ambapo angependa kuona watalii wengi zaidi kutoka China wanatembelea Zanzibar na kwa wawekezaji kuangalia fursa za kujenga hoteli kubwa za watalii.
Kwa upande wa uvuvi amewakaribisha kuwekeza katika eneo la uvuvi wa bahari kuu na uvuvi wa kawaida kwani soko la bidhaa za bahari ni kubwa hata kwao .
Pia aliwaalika kuangalia uwezekano wa kushiriki katika mradi wa mafuta na gesi kutokana na ubobezi wao katika sekta hiyo.
Maeneo mengine Dk Mwinyi aliyowaalika wawekezaji hao ni katika ujenzi wa Bandari kubwa ya Mangapwani itakayohudumia nchi nyingi za Afrika. Kwa upande wa Tanzania Bara amewaalika wawekezaji hao kwenye kilimo kwani kuna ardhi kubwa yenye rutuba.
Hata hivyo wawekezaji hao walivutiwa zaidi na sekta ya mafuta na gesi na wameonesha utayari wao kujitosa kwenye mradi huo kwani kwa China kampuni yao ni ya tatu kwa ukubwa kwenye sekta ya mafuta.
Pia Dk. Mwinyi alikutana na Rais wa Kampuni ya China Civic Engineering Construction Corporation- CCECC. Hii ni kampuni kubwa ya ujenzi yenye miradi 27 ya ujenzi wa barabara Tanzania.
Rais Dk. Mwinyi alionesha kuridhishwa na kasi na uwezo mkubwa wa kampuni hiyo kwenye miradi ya barabara Zanzibar akitolea mfano barabara ya Kaskazini Unguja ambayo ni bora sana.
Ameiomba kampuni hiyo kusaidia kurudishwa kwa mikopo kutoka taasisi za fedha zikiwemo benki. Mikopo hiyo ilisimamishwa baada ya kuzuka ugonjwa wa UVIKO 19.
Katika mazungumzo mengine aliyofanya Dk. Mwinyi na wawekezaji waliojikita zaidi katika kilimo na hawa ni akina mama ambao walimuomba Rais eneo kilimo Zanzibar.
Hata hivyo Dk Mwinyi aliwafahamisha kwamba Zanzibar haina eneo kubwa linalofaa kwa kilimo na akawaelekeza kwenda kulikagua shamba la Bagamoyo la Makurunge ambalo ni mali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wawekezaji hao wa Kampuni ya Longping High Tech wameafiki kwenda kulikagua eneo hilo la Makurunge mwezi Agosti mwaka huu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi atamaliza ziara yake nchini China kesho Jumamosi kurudi nyumbani.
Comments are closed.