Dk Mwinyi aongoza Tamasha la Mazoezi

ZANZIBAR: RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amewahimiza viongozi na wananchi kufanya mazoezi ili kulinda afya na kujikinga na maradhi yasiyoyambukiza kwa kutenga muda wa dakika thelathini kwa angalau siku tatu kwa juma.

Dk Mwinyi amesema hayo Januari Mosi, 2024 katika Tamasha la Mazoezi ya Viungo kitaifa lililoshirikisha vilabu 149 kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara kwa matembezi yaliyoanzia Mnarani Kisonge mpaka Uwanja wa Amaan Mkoa wa Mjini Magharibi.

“Kama tujuavyo tunaelekea kwenye kilele cha sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, ambapo tamasha la leo ni miongoni mwa shamrashamra za kilele hicho,” amesema kiongozi huyo.

Amewaasa wananchi kulinda miundombinu ya Serikali ikiwemo viwanja vya kisasa vya michezo vilivyoboreshwa, ikiwemo viwanja vya Amaan Complex vya mjini Unguja na vile vya Gombani, Pemba.

Aidha, kiongozi huyo amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inahimiza wananchi kushiriki katika usafi kwani usafi ni afya na ameitaka jamii kushiriki mazoezi na michezo ili kujiepusha na vitendo viovu na kujihadhari na magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza.

Habari Zifananazo

Back to top button