Dk Mwinyi apongezwa nia kubinafsisha mashirika

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi

WADAU wa sekta binafsi na wachumi wamesema Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ana lengo sahihi kutaka kuyakabidhi mashirika ya umma kwa sekta binafsi kama yanashindwa kujiendesha kwa faida.

Wamesema sekta binafsi wana mtaji, teknolojia na hawana kikwazo kuingia ubia na mtu mwingine kwa urahisi ikilinganishwa na serikali.

Hivi karibuni, Dk Mwinyi aliagiza mashirika ya umma yajitathmini, yaweke mikakati ya kuleta mabadiliko ya haraka na hataki kuona yanapata hasara.

Advertisement

Alisema kama serikali itashindwa kuyaendesha, yatakabidhiwa kwa sekta binafsi ili yajiendeshe kwa faida.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Nebart Mwapwele alisema hiyo ni fursa kwao na itaongeza tija kwa sekta binafsi.

Mwapwele alisema serikali inapaswa kubaki kusimamia na kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji na sekta binafsi iachwe itekeleze masuala ya uwekezaji.

“Kwa hiyo hilo wazo la Rais ni zuri na kama litafanyika litaongeza tija. Serikali ibakie na jukumu la kutengeneza mazingira, kuratibu na kusimamia, na sekta binafsi ndiyo iingie kwenye uendeshaji wa shughuli za uchumi yakiwemo mabenki, viwanda na taasisi za uzalishaji,” alisema Mwapwele.

Kwa mujibu wake, kinachosababisha hasara kwenye mashirika ya umma mara nyingi ni ukosefu wa mipango kwa kuwa mengi yanajiendesha kwa kutegemea ruzuku ya serikali hivyo inapoondolewa yanashindwa kujisimamia.

Alisema ni vyema serikali ikubali mashirika hayo yaendeshwe na wataalamu wenye sifa ya kuyaendesha na ikubali yaingie ubia kwa kuwa dunia ya sasa mambo yanafanyika kwa kuunganisha nguvu ikiwamo mitaji.

Mtaalamu wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi alisema amefanya utafiti kwenye mashirika ya umma tangu mwaka 1977.

Alisema wamebaini kuwa mashirika ya umma yanatakiwa kufanya kazi kibiashara kwa kutumia mbinu za sekta binafsi za kuyawezesha kupata faida vinginevyo yataendelea kuwa mzigo kwa serikali.

“Maana mashirika ya umma yamechukuliwa kama vile biashara ambayo kila mtu anaweza kuamua kumpeleka mtu wake kufanya kazi, matokeo yake badala ya kuajiri watu 10 unajikuta unaajiri watu 20 na matokeo yake kazi haifanyiki,” alisema Profesa Moshi.

Alisema pia yanapaswa kutumia mbinu za sekta binafsi ikiwamo ya kuwapata mameneja kwa kuzingatia uwezo na sifa zinazotakiwa kwa njia ya ushindani.

Aidha, alisema ni muhimu mashirika ya umma yapewe uhuru wa kuendesha bila kuingiliwa na serikali kwa kuamuliwa mambo ya kufanya.

Alisema ni muhimu pia yaajiri watu wenye sifa na yasilazimishwe kununua bidhaa au vitu kwa mtu fulani au kampuni fulani kwa bei badala ya kununua kwenye bei ya soko.

 

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *