RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametaka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) watumie vizuri demokrasia kwa kuchagua viongozi kwa busara na kuzingatia wanachama wenye uwezo, uadilifu na wanaokataa rushwa.
Taarifa ya Idara ya Mawasiliano Ikulu Zanzibar ilieleza kuwa Dk Mwinyi alisema hayo Jumapili aliposhiriki katika Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa CCM ngazi ya jimbo uliofanyika ofisi za Jimbo la Mpendae, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika mkutano huo wajumbe walipata fursa ya kupiga kura na kuchagua viongozi katika nafasi ya Mwenyekiti wa Jimbo, Katibu wa Jimbo na Katibu wa Siasa na Uenezi wa Jimbo hilo.
Nafasi nyengine zilizogombewa ni wajumbe watatu wa Mkutano Mkuu wa Mkoa, wajumbe watano wa Halmashauri Kuu ya Wilaya na wajumbe watano wa Halmashauri Kuu ya jimbo.
Wakati huohuo taarifa hiyo ilieleza pia Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kwa nyakati tofauti wameifariji familia ya Rais Mstaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi kutokana na kifo cha mwanawe,Hassan Ali Hassan Mwinyi kilichotokea Jumatano wiki hii katika Hospitali ya Mnazi mmoja, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo dua ilifanyika nyumbani kwa marehemu Chukwani Mkoa Mjini Magharibi ambako viongozi hao pia walipata fursa ya kutoa mkono wa pole kwa mzee Mwinyi, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Mama Siti Mwinyi, mke wa marehemu , Fauzia Salim Hilali na wanafamilia.