RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amemuapisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA), Ali Abdalla Ali na kumpa majukumu matatu likiwemo la kufanya uchunguzi katika Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ambako imebainika kuna upotevu wa fedha.
“Nakushukuru kwa kupokea uteuzi wangu ambapo majukumu ni makubwa, lakini nataka uende ukafanye kazi kwa kushirikiana na vyombo vya uchunguzi…nataka uende ukafanye kazi katika maeneo matatu makubwa ili tujue fedha za serikali zimepotea wapi,” alisema Dk Mwinyi.
Alisema Ali anapaswa kuifanyia kazi ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu ya mwaka 2021-2022 ili kuelewa matokeo yake wakiwemo waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria.
Pia alimuagiza afanye kazi kwa karibu na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuhakikisha waliohusika wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria ambapo ni mahakama.
Dk Mwinyi alisema serikali imejipanga kuwatumikia wananchi kwa kuwafikishia maendeleo na matukio ya wizi yanayotokea ni hatari kwani serikali itashindwa kutekeleza wajibu wake.
“Huu ni wakati wa kukomesha wizi na ubadhirifu serikalini…tusipokomesha tutashindwa kuwatumikia wananchi katika yale mambo ambayo tumewaahidi,” alisema.
Aidha, Dk Mwinyi alimuahidi Ali kwamba serikali itaijenga upya taasisi hiyo ili iwe na uwezo kikamilifu wa kupambana na rushwa na kudhibiti wizi na upotevu wa fedha serikalini.