Dk Mwinyi ataka ufanisi Uwanja Ndege Z’bar

Dk Mwinyi ataka ufanisi Uwanja Ndege Z’bar

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amewaagiza watendaji wa Serikali wanaohudumu Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, waendane na kasi ya wawekezaji ili kuimarisha huduma kwa raia wa kigeni.

Dk Mwinyi ametoa maagizo hayo wakati akifungua maduka na huduma za kampuni ya kimataifa (DNATA), kwenye jengo jipya la Terminal 3 uwanjani hapo.

Aliitaka Idara ya Uhamiaji Zanzibar, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wahudumu wa afya na benki kutumia mifumo ya kisasa kuimarisha huduma zao, ili kuwaondolea usumbufu wageni wanaokaa muda mrefu kusubiri huduma.

Advertisement

Alisema serikali imepata mafanikio kupitia wageni mbalimbali wanaoingia nchini na kutunisha kipato chake na kufikia Sh billioni 8.1 kutoka kwenye robo ya kwanza na ya pili ya mwaka wa fedha 2022/2023 (Julai -Desemba), ikilinganishwa na makusanyo ya robo ya pili mwaka 2019 ambayo yalikuwa Sh billioni 2.5.

Kwa mwaka 2022 idadi ya abiria ilifikia milioni 1.8 ikilinganishwa na milioni 1.3 kwa mwaka 2021, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 38.