Dk Mwinyi ataka Watanzania kutumia fursa za AGRF

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewataka Watanzania kutumia fursa ya Jukwaa la Mifumo ya Chakula la Afrika kwa mwaka 2023 (AGRF), linalofanyika nchini, kutangaza fursa za kilimo zilizopo hali itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ajira.

Rais Mwinyi aliyasema hayo katika uzinduzi wa jukwaa hilo uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Alisema Tanzania ina fursa kubwa ya uwekezaji katika sekta ya kilimo hivyo ni matumiani kuwa jukwaa hilo litatoa nafasi nzuri kuzifafanua kwa kina fursa hizo kwa dunia na kuvutia uwekezaji.

Alisema kuwepo kwa jukwaa hilo nchini kunadhihirisha utashi na dhamira aliyonayo Rais Samia Suluhu Hassan kuwakomboa Watanzania kwa kutengeneza ajira miongoni mwa vijana na wanawake katika sekta ya kilimo.

Alieleza kuwa hatua hiyo ni namna bora ya kuzitumia rasilimali mbalimbali zilizopo nchini ikiwemo ardhi kubwa yenye rutuba na mifugo mingi.

“Hatuna shaka kwamba jukwaa hili litafungua fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya kilimo na hivyo kutoa ajira nyingi kwa wananchi wetu kupitia kilimo cha mkataba na fursa za masoko na bidhaa zinazozalishwa nchini.

Dk Mwinyi alisema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya uchaguzi imeahidi kutoa ajira milioni tatu kwa Tanzania Bara na 300,000 Zanzibar na kwamba hakuna sekta itakayotuwezesha kufikia hayo zaidi ya sekta ya kilimo.

Alimshukuru Rais Samia kwa wazo zuri la kuifungua nchi na kuvutia uwekezaji katika sekta ya kilimo.

“Sisi kule Zanzibar watu wetu wengi wameajiriwa au kujiajiri katika eneo la uvuvi au kilimo cha mwani. Na katika kilimo cha mwani karibu asilimia 90 wanaofanya kazi hiyo ni wanawake. Kwa hiyo tutakuwa tayari kuja kuonesha fursa nyingi tulizokuwa nazo katika eneo la kilimo na uvuvi,” alisema.

Alisema sekta hiyo itawezesha kuajiri watu wengi hususani vijana na wanawake.

“Leo kuna vijana wengi wanaoshindwa kuendelea na vyuo na wanaomaliza hawana ajira, tuna imani uwekezaji katika sekta hii utatoa ajira nyingi kwa vijana hawa,” alisema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button