RAIS wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi ametaka madhimidho ya Siku ya Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani yatumike kama fursa ya kuweka mkazo katika Uhuru wa kujieleza ndani ya ajenda ya jumla ya haki za binadamu.
Rais Mwinyi ameyasema hayo leo Mei 3, 2023 mjini Zanzibar katika maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, ambapo yeye alikua mgeni rasmi
Amesema jumuiya za kimataifa na wadau mbalimbali wa habari watumie siku hiyo kujadiliana na mashirika mbalimbali kama vile mazingira, haki za wanawake na haki za watoto, ili kutangaza habari zinazohusu masuala hayo.
Amesema, serikali zote mbili zitaendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vyote vya habari katika kuhakikisha serikali inatatua changamoto zinazowakabili wanahabari .
“Katika kuadhimisha miaka 30 ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, niwaombe ndugu zangu wanahabari tuendelee kuwa wazalendo kwa nchi yetu, hakuna uhuru usio na mipaka lakini pia hakuna uhuru usio na wajibu,” amesema Dk mwinyi.
Amesema usajili wa vyombo vipya vya habari nchini umeongezeka kwa kasi kubwa jambo lililofanya uhuru wa kujieleza na kusambaza habari nao umeongezeka.
“Usajili mkubwa wa vyombo vya habari umeonekana zaidi mwaka 2020 na 2023 ni ukweli usiopingika kuwa sheria, kanuni na taratibu zetu ndizo zinazoruhusu uwepo wa vyombo hivyo,” amesema Rais Mwinyi
Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Tabia Maulid Mwita amesema mchakato wa sheria ya habari Zanzibar umefikia asilimia 80 na kuwataka wadau wa habari Zanzibar kuwa na subira.
“Serikali yenu ni sikivu, tunawahakikishia kuwa na sheria nzuri zitakazokidhi matakwa, tutauwasilisha Baraza la Wawakilishi na taratibu nyingine ziendelee,”amesisitiza.