Dk Mwinyi awataka mabalozi waibebe nchi

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewataka na kuwapa mbinu mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania kwenye mataifa mengine wahakikishe wanapotekeleza majukumu yao, vipaumbele vyao viendane na vya serikali zote mbili na waitangaze nchi kimkakati.

Kauli hiyo aliitoa jana katika Ukumbi wa Golden Tulip, Kiembe Samaki, Unguja, alipokutana na kuzungumza na mabalozi zaidi ya 40 wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali na jumuiya za kimataifa.

Mabalozi hao wako Zanzibar wakiendelea na mkutano wao ulioitishwa na Rais Samia Suluhu Hassan na utamalizika kesho Novemba 20, kisha mabalozi hao kurejea kwenye vituo vyao vya kazi.

Akizungumza na mabalozi hao, Dk Mwinyi alisema ni fursa nzuri ya kuangalia mwenendo mpya katika kuimarisha demokrasia, kuangalia vipaumbele vya serikali, kueleza mambo yaliyoboreshwa na wajibu wa mabalozi hao katika kuhakikisha wanaitangaza Tanzania ili kuleta tija ya diplomasia ya uchumi.

“Ni muhimu mhakikishe vipaumbele vyenu vinaendana na vipaumbele vya serikali zenu mbili na zingatieni ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inahimiza kuna haja ya kutoa ushirikiano na kufanya kazi kwa karibu na serikali zenu. Tafuteni masoko, biashara na kuitangaza nchi ili muongeze idadi ya watalii na uwekezaji,” alisema.

Dk Mwinyi alielezea maboresho yaliyofanywa na serikali ya Zanzibar na kutaka mabalozi hao kuyachukua na kwenda kuyatangaza ili mataifa yajue na kushawishika kuja kuwekeza visiwani humo.

Alisema hatua zilizochukuliwa na serikali ni pamoja na kuboresha huduma za umeme, maji, viwanja vya ndege na sasa Zanzibar inapokea idadi kubwa ya watalii kuliko viwanja vyote vya ndege nchini.

Akizungumzia sekta ya utalii, Dk Mwinyi alisema baada ya miaka kadhaa ya changamoto za majanga yakiwemo ya athari za Covid-19, hali sasa ni shwari na utalii umerejea kwa kasi.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa kwa mwezi mmoja wa Agosti mwaka huu, Zanzibar ilipokea watalii 61,388 ikilinganishwa na mwaka jana ambao walikuwa 34,000.

Aidha, kwa kipindi cha miezi minane kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu, Zanzibar ilipokea watalii 322,748, sawa na ongezeko la asilimia 27.6 ikilinganishwa na mwaka jana na kwamba watalii walioongoza walitoka ukanda wa Ulaya kwa asilimia 70 ya watalii wote.

“Niwapongeze wadau na mabalozi wetu kwa kuunganisha Zanzibar na watalii kuja kutembelea na kufanya matamasha makubwa hapa. Niombe mabalozi mwendelee kushirikiana na taasisi za utalii kuitangaza nchi ili idadi ya watalii izidi kuongezeka,” alisema.

Aliwaeleza mabalozi hao kuwa Zanzibar imejipanga kuongeza idadi ya watalii kutoka 538,000 mwaka 2019 hadi wafike 850,000 mwaka 2025 na kwamba ofisi za ubalozi na mabalozi wana nafasi kubwa ya kuchangia na likatekelezeka.

Vilevile Dk Mwinyi aliwaeleza kuwa serikali ya Zanzibar imekamilisha mpango wa kujenga bandari jumuishi -MangaPwani, itakayohusisha bandari ya mizigo, mafuta, gesi, uvuvi na nafaka na kuwa jitihada hizo zinaenda sambamba na kuimarisha bandari za Malindi mkoani Pemba na nyingine visiwani humo.

Alisema maboresho mengine yanayofanywa ni mazao ya kimkakati ambayo ni viungo, mwani na karafuu na kuwa jitihada zimefanywa kuongeza uzalishaji wake na kuyasindika na dhamira ya sasa ni kuhakikisha viwanda vya kuongeza thamani mazao hayo vinajengwa ili mkulima auze bidhaa zenye thamani zaidi.

“Kwenye hili niwaombe mabalozi msaidie kupata teknolojia hizo za viwanda vya kuongeza thamani mazao hayo, ili uchumi wa wananchi wetu ukue zaidi, lakini pia mnaporudi nendeni mkaseme haya tunayoboresha ili kuwashawishi wawekezaji na wafanyabiashara waje kuwekeza Zanzibar,” alisema.

Awali Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab alisema maudhui ya mkutano huo wa mabalozi ni kujadiliana na kubadilishana uzoefu na kupokea maekelezo kutoka kwa viongozi wakuu wa nchi.

Alisema kaulimbiu ya mkutano huo ni ‘Mwelekeo mpya katika kuimarisha diplomasia ya uchumi’ na kuwa imelenga kuchagiza utekelezaji wa sera ya mambo ya nje na kutoa msukumo mpya wa utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

Balozi Fatma alisema katika mkutano huo wa mabalozi mada mbalimbali zimetolewa na baadhi ni fursa na mikakati ya kuiwezesha Tanzania kunufaika na eneo Huru la Afrika, (AfCFTA), mwelekeo mpya kuimarisha diplomasia ya uchumi na fursa za uchumi Zanzibar.

Akizungumza kwa niaba ya mabalozi, Amidi Mkuu wa Mabalozi hao, Balozi AshaRose Migiro alisema mkutano huo umetoa fursa kwa mabalozi kujadili fursa zilizopo na jinsi ya kunufaika nazo.

Katika mada zilizotolewa, baadhi zilihusu mwenendo wa dunia na taswira yake katika diplomasia ya uchumi, mabadiliko yaliyotokea anga za kimataifa na athari zake katika biashara za kimataifa, mabadiliko ya tabianchi na fursa zilizopo, mapinduzi ya nne ya viwanda na kwamba wamejadili haja ya kuwa na mwelekeo mpya wa kutekeleza diplomasia ya uchumi.

“Tumeelezwa Zanzibar imejipanga kutumia fursa katika maeneo makuu matatu ya ushirika wa kikanda ambayo ni uhuru wa watu, mawasiliano na urahisi wa kutumia sarafu za nje na sisi tunasema kimbilio letu la kwanza ni ushirikiano wa kikanda na tutaendelea kuangalia mbele zaidi,” alisema Dk Asha-Rose Migiro.

Alisema wao kama mabalozi wametambua fursa zilizopo Zanzibar na kuahidi kwamba watatafuta ubia na wawekezaji ili wawekeze kwenye uchumi wa buluu ambao ni muhimu hivi sasa kwa maendeleo ya Zanzibar.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax alisema mkutano huo umetoa fursa kwa mabalozi kukutana na viongozi wa nchi na kujadili masuala mbalimbali muhimu.

Habari Zifananazo

Back to top button