RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema hakuna sababu ya mashirika ya umma kupata hasara hivyo yajitathmini na kuweka mikakati ya mageuzi ili kuwe na mabadiliko ya haraka.
Dk Mwinyi alisema hayo Ikulu Zanzibar alipozungumza na watendaji wakuu wa mashirika hayo na akaagiza wafanye maboresho ya kiutendaji.
Aliagiza mashirika yanayotoa huduma kwa wananchi yazitumie changamoto zinazowakabili ziwe fursa zenye tija ili kuleta mabadiliko chanya ikiwa ni pamoja na kubadili mifumo ya taasisi zao.
Akiizungumzia Mamlaka ya Maji Zanzibar, (ZAWA) na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Dk Mwinyi aliagiza watendaji wa mashirika hayo wajitathmini na huduma wanazowapatia wananchi na kwa nini wakose faida.
Aidha, aliwashauri ZAWA waache kutumia pampu zinazotumia umeme wa ZECO badala yake watumie za umeme wa jua ama solar ili kukwepa matatizo ya kuungua kila mara na kuwaondolea wananchi shida ya kukosa maji mara kwa mara.
Aliyashauri mashirika yanayojitegemea kutafuta mitaji kuwekeza kwenye uzalishaji wenye faida kwa mustakabali wa mashirika hayo na serikali kwa ujumla.
Alisema kama serikali inashindwa kuyaendesha ili kuepuka hasara, alishauri wapewe sekta binafsi ili serikali ipate faida na wananchi wapate huduma wanazostahiki.
Akiyazungumzia mashirika ya umma yanayojiendesha kama Shirika la Bima, ZMUX na mengine, alishauri kutafuta mitaji na kujiendesha kibiashara hususan ZMUX ili kuendana na soko la ushindani.