Dk Mwinyi: Kiwanda cha mwani mageuzi makubwa kiuchumi

ZANZIBAR: RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema ujenzi wa kiwanda cha kusarifu na kuongeza thamani ya mwani ni sehemu ya mikakati ya mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa wakulima wa zao hilo linalolimwa na wanawake kwa asilimia 90.

Akiweka jiwe la msingi katika kiwanda cha mwani Chamanangwe Mkoa wa Kaskazini Pemba jana, Dk Mwinyi alisema kiwanda hicho ni mkombozi kwa wazalishaji wa zao hilo ambacho ni cha kwanza katika Afrika Mashariki na Kati.

Hivyo, alisema huu ni wakati mwafaka kwa wakulima kuongeza uzalishaji wake kufikia mahitaji ya soko.

Alisema hiyo ni sehemu ya mikakati ya kukifungua Kisiwa cha Pemba kiuchumi na uwekezaji na kuwa eneo la Chamanangwe ni maalumu kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya aina mbalimbali.

Aliwataka wakulima wa maeneo mengine ya mwambao wa Pwani ya Tanzania Bara ikiwamo Tanga hadi Mtwara, kutumia fursa za uzalishaji wa mwani kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya zao hilo.

“Hiki ni kiwanda cha kwanza Afrika ya Mashariki ambapo changamoto kubwa ni kuyafikia malengo na mahitaji yake ni wastani wa tani 30,000 na sasa tunazalisha tani 20,000,” alieleza Dk Mwinyi.

Alisema serikali imeunda kampuni ya mwani kuratibu na kuangalia mwenendo wa maendeleo ya zao hilo ikiwemo kuwepo kwa bei nzuri kwa wakulima.

Alisema alipata taarifa kwamba tayari kampuni ya mwani imeanza kununua zao hilo kwa wakulima kwa bei, ambayo ni tofauti na ile inayotolewa na kampuni binafsi.

“Nimepata taarifa ya kuanza kununua mwani kwa wakulima kwa bei tofauti ambapo mwani mwembamba unanunuliwa kwa bei ya Sh 1,000 na ule mnene kwa Sh 2,000,” alisema.

Waziri wa Maendeleo ya Biashara na Viwanda, Omar Said Shaaban alisema ujenzi wa mradi huo ni matokeo ya ubunifu wa Rais Mwinyi katika matumizi ya fursa za uchumi wa buluu na kuwaneemesha wananchi.

Aliwataka wakulima kuongeza kasi ya uzalishaji kwa ajili ya kufikia mahitaji yake ambako kiwanda hicho kinahitaji jumla ya tani 30,000 kwa mwaka.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mwani (ZASCO), Masoud Rashid alisema ujenzi wa kiwanda cha kusarifu na kuongeza thamani kinatarajiwa kugharimu jumla ya Sh bilioni 7.4, na kitajengwa kwa awamu mbili tofauti.

Alisema ujenzi huo utaongeza thamani ya zao la mwani pamoja na bei yake kuongezeka kutoka kwa wakulima na hivyo kuinua hali za kiuchumi kwa wazalishaji wake ambao asilimia 90 ni wanawake.

Aliwataka wakulima kulima mwani kwa wingi kukidhi mahitaji ya kiwanda katika soko la ndani na nje ya nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib alisema kuwepo kwa kiwanda cha kusarifu na kuongeza thamani ya zao la mwani kwa kiasi kikubwa ni sehemu ya fursa ya kuwawezesha wanawake kunyanyua hali zao kiuchumi.

Habari Zifananazo

Back to top button