Dk.Ndumbaro:fanyeni kazi saa 24
DAR ES SALAAM: Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk.
Damas Ndumbaro amemuagiza Mkandarasi wa Ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa Beijing Construction Engineering Group (BCEG) kufanya kazi hiyo, kwa saa 24 na siku zote za wiki ili kazi hiyo ikamilike kabla ya Oktoba 15, 2023.
–
Dk. Ndumbaro ametoa maagizo hayo Septemba 13, 2023 jijini Dar es Salaam mara baada ya kupokea taarifa ya ukarabati wa uwanja huo pamoja na ujenzi wa eneo changamani la viwanja vya michezo unaoendelea katika eneo hilo.
–
Akiwa uwanjani hapo Dk. Ndumbaro amekutana na baadhi ya Wataalam kutoka African Football League ambao wamewasili nchini kwa ajili ya ukarabati katika maeneo ambayo watafanya kwa gharama zao.
–
Awali Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Saidi Yakubu ameeleza kuwa, vifaa vya Benchi la Ufundi ambavyo vinasimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwenye ukarabati huo tayari vipo njiani kuwasili nchini.
–
Amesema taa za uwanja huo zipo njiani na zitafungwa mapema kabla ya mechi ya ufunguzi wa African Football League Oktoba 20, 2023 pamoja na vifaa vya ukarabati wa eneo la kuchezea ambao utafanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
–
Aidha, Dk. Ndumbaro amekagua ukarabati wa Uwanja huo pamoja na mradi wa ujenzi wa viwanja vya michezo na kupumzikia vinavyojengwa katika eneo changamani la michezo la jijini hapo.