WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia miongoni mwa jamii ya Watanzania havikubaliki.
Dk Ndumbaro aliyasema hayo wakati wa kufanya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa kampeni ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria.
Kampeni hiyo inayofanyika nchi nzima kwa miaka mitatu, imelenga kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria.
Alisema siku za karibuni kumekuwapo ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili wa kijinsia na kusisitiza kuwa vitendo hivyo ni uvunjaji wa sheria.
Dk Ndumbaro alisema nchi imeingia kwenye kadhia kubwa na ndio maana Rais Samia amewatuma kuzungumza na wananchi kuwaambia kuwa ukatili wa kijinsia haukubaliki na kuwa ndio maana serikali imeanza kutoa elimu ya msingi ya sheria ili watoto, dada na wajukuu.
“Mtu anabaka na kulawiti watoto, huo ni ukosefu wa maadili na ni laana kubwa ambayo haiungwi mkono na dini yoyote, mbaya zaidi ni ukiukwaji wa sheria na unakuwa umetenda kosa la jinai.
“Ukishafanya hivyo basi utakamatwa na kupelekwa mahali unapostahili maana huwezi kuishi sehemu ya wastaarabu,” alisema.
Dk Ndumbaro alisema changamoto nyingine ni mirathi ambapo wanawake wengi wamekuwa wakinyang’anywa mali na kusisitza kuwa vitendo hivyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Kuhusu malalamiko ya wananchi kuhusu kudhulumiwa ardhi, Dk Ndumbaro aliwahidi wananchi kutuma timu maalumu ambayo itaweka kambi wilayani Kondoa kwa ajili ya kusikiliza na kutatua changamoto hiyo.
“Kwa watu niliowasikiliza inaonekana migogoro ya ardhi ni changamoto kubwa hapa, inaonekana tatizo kubwa ni ofisi ya ardhi katika halmashauri, mimi niwaahidi kuwa tutaleta timu maalumu wiki ijayo ije ipitie changamoto hizi na zingine ambazo hazijasemwa.”
“Kama mwananchi ametoa eneo kwa ajili ya maendeleo na si kuchukuliwa na mtu binafsi, sheria iko wazi kuwa anapaswa kulipwa fidia na suala la fidia sio siri kwani sheria inasema wazi alipwe kiasi gani,” alisema.
Alisema baada ya timu hiyo kumaliza kazi, Dk Ndumbaro aliwaahidi kurejea tena hapo akiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kamishina wa Ardhi na Mbunge lengo likiwa ni kujiridhisha na kuhakikisha changamoto za wananchi zimetatuliwa zote.
“Na kama tutathibitisha kuna mtumishi anawavuruga wananchi, basi sisi tutaondoka naye na kumpeleka anapostahili. Hatutakubali watu waliopewa dhamana ya kusimamia maslahi ya wananchi ndio wanakuwa wa kwanza kudhulumu haki za wananchi,” alisema.