MWANADIPLOMASIA mashuhuri nchini, Balozi Salim Ahmed Salim anatarajia kupokea tuzo ya Kigoda cha Mwalimu Nyerere na Umajimui wa Kiafrika yenye lengo la kuutambua na kuuthamini mchango mkubwa alioutoa kwa taifa.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Rwekaza Mukandala alisema hayo wakati akielezea tuzo hiyo itakayotolewa kesho katika Tamasha la Kigoda hicho lililoanza leo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Profesa Mukandala alisema jopo la majaji limemchagua Salim kutokana na kuwa mwanadiplomasia tangu akiwa na miaka 21 ambapo aliiwakilisha Tanzania nchi za Misri na baadaye India.
“Baada ya hapo Salim alikuwa Umoja wa Mataifa, aliporudi akawa Katibu Mkuu wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU), baadaye Waziri Mkuu wa Tano wa Tanzania baada ya kifo cha Edward Sokoine mwaka 1984 hadi 1985”.
“Amefanya shughuli nyingi kitaifa na kimataifa na ametambulika kimataifa na kitaifa kwa hiyo tunaona ni mtu anastahili, ni muumini mkubwa wa fikra za mwalimu (Nyerere), anasimamia, amezitekeleza ametetea nchi yetu kwa miaka mingi”.
“Amesimamia vizuri, amekuwa ni msomi hakuogopa kubadilishana mawazo katika mihadhara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, vigoda vilivyopita alishiriki hivyo tumeona inamfaa, kwa hiyo jopo la majaji limeona apewe hiyo tuzo,” alisema.
Mbali na tuzo hiyo ya Mwalimu, Mukandala alisema kuwa tangu kigoda hicho kimeanza wameanzisha klabu za mwalimu katika shule mbalimbali za sekondari, juhudi ambazo zinaendelea mpaka sasa.
Alitaja mikoa ambayo zipo klabu hizo kuwa ni Mwanza, Geita, Kagera, Dodoma, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam na Mtwara, juhudi zaidi zinaendelea katika mikoa mingine.
Pia alisema UDSM kuna kozi maalumu zilizoandaliwa katika mitaala kwa ajili ya kufundisha vizuri mawazo na fikra za mwalimu Nyerere.
Alisema kigoda hicho kinafanyika kwa mara ya 14 sasa kwa ajili ya kuendeleza na kuenzi fikra za muasisi wa taifa Mwalimu Nyerere, aliyekuwa baba wa taifa, na Mkuu wa UDSM wa kwanza katika kuendeleza fikra zake nzuri, adimu na muhimu katika kudumisha umoja, utaifa na maendeleo ya nchi.
“Mwalimu aliamini katika uajumui wa Afrika kuwa lazima ili Tanzania iwe na nguvu lazima tuwe hivyo kwa kuungana na nchi za Afrika na kushirikiana,” alisema.