WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 42 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika unaofanyika Addis Ababa.
Mkutano huo unaofanyika leo na kesho ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika utakaofanyika Februari 18-19, 2023.
Pamoja na mambo mengine, mkutano wa Mawaziri utajadili masuala ya kimkakati yanayohusu Bara la Afrika, ikiwemo utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika-AfCFTA, uhakika wa chakula, hali ya ulinzi na usalama, mabadiliko ya tabianchi, pamoja na masuala ya kiutawala na usimamizi wa rasilimali za Umoja wa Afrika.
Akichangia katika mkutano huo, Dk Tax alisisitiza umuhimu wa Kamisheni na Taasisi za Umoja wa Afrika kusimamia vyema rasilimali za Umoja wa Afrika kwa kuchukua hatua za kuondoa mapungufu yaliyobainika kwenye taarifa ya ukaguzi wa rasilimali za Umoja wa Afrika.
Waziri pia alieleza hatua ambazo Serikali ya Tanzania inachukua katika kutekeleza mikataba ya Uenyeji ya Taasisi za Umoja wa Afrika zilizopo Tanzania, ambazo ni Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Umoja wa Posta Afrika na Bodi ya Umoja wa Afrika ya Ushauri dhidi ya Rushwa.
Awali akiwasilisha hotuba yake ya ufunguzi, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Moussa Faki Mahamat alisisitiza umuhimu wa Umoja wa Afrika kuendelea kutoa kipaumbele kwenye masuala yanayowagusa wananchi wa Afrika, ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za mabadiliko za kijamii, kiuchumi na kiusalama.
Alisisitiza umuhimu wa Afrika kupunguza utegemezi wa chakula kutoka nje kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa za vyakula ndani ya bara la Afrika pamoja na kutumia fursa za mkataba wa AfCFTA katika kukuza Mtangamano wa Kiuchumi.