RAIS Samia Suluhu Hassan tayari amewasili Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kutangaza matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 iliyofanyika kuanzia Agosti 23 mwaka huu.
Uwanja wa Jamhuri umefurika watu wa rika mbalimbali kuanzia asubuhi, huki wengi wakionekana kuwa na shauku ya kusikia kile kitakachosemwa.
Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini, kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalumu.
Sensa hufanyika kila baada ya miaka 10, ambapo sensa ya mwaka 2022 ni ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.
Matokeo ya sensa ya mwaka 2012 yalionesha kuwa Tanzania ilikuwa na watu 44,929,002 wakiwamo 43,625,434 Tanzania Bara na 1,303,568 Zanzibar.