Dodoma kutumia takataka kutengeneza gesi, mbolea

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeingia mkataba na kampuni kutoka nchini Zimbabwe itakayokuwa ikichakata taka kutoka kwenye dampo na kupatikana kwa gesi na mbolea.

Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe alisema hayo jana wakati wa zoezi la usafi lililofanyika kwenye soko la Bonanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya usafi wa mazingira kitaifa.

Alisema Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeingia mkataba na kampuni kutoka nchini Zimbabwe itakayokuwa ikichakata taka katika dampo kuu lililopo eneo la Chidaya na kupatikana kwa gesi na mbolea.

Alisema uchakataji huo utafanya takataka zinazokusanywa kuwa sehemu ya fursa ya kiuchumi.

Pia alisema wananchi wengi wa Dodoma wanapenda usafi na kutunza mazingira ila jambo linalotakiwa ni kuratibu kazi zao.

“Kwa uongozi wa soko, uongozi wa mtaa kuhakikisha wanaweka usimamizi, usafi ni tabia, ni vyema kwa wananchi wakawa na tabia ya kufanya usafi kwenye maeneo yao,” alisema.

Pia aliagiza wananchi walioweka makalavati mbele ya mitaro wayavunje ili ipitishe maji.

“Kama wanataka kuweka madaraja karibu na sehemu zao za biashara waweke ya vyuma kwani hayo yana uwezo wa kupitisha maji, wafanye hivyo mara moja kwani nitapita kukagua kama yametolewa,” alisema.

Diwani wa Kata ya Chamwino, Jumanne Ngede alisema kuwa kata hiyo inashika nafasi ya sita kwenye usafi.

“Tumechukua maagizo ya Meya ya makalavati yaliyojengwa kwenye mitaro ya kupitisha maji ya mvua yabomolewe ili maji yapite yasituame, tutalisimamia hilo,” alisema.

Alisema wananchi wamekuwa wakijitokeza kufanya usafi lakini mikakati zaidi inahitajika ili wananchi wabadili mitazamo na kuona kuwa suala la usafi ni muhimu kwa kila mmoja.

Kaimu Mkurugenzi Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Dk Beatrice Mutayoba alisema kuna mwitikio mkubwa wa watu kujitokeza kufanya shughuli za usafi unaosaidia kutunza vyanzo vya maji ardhini na manufaa mengine.

Habari Zifananazo

Back to top button