TAASISI ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imewasilisha taarifa ya utafiti wa madini yanayopatikana nchini Tanzania huku Dodoma ikiongoza kwa kuwa na orodha ya madini ya aina nyingi.
Akiwasilisha taarifa jana Julai 28, 2023 Meneja Jiolojia kutoka, Maswi Solomon amesema utafiti huo umeonesha kuwa miongoni mwa madini matano ya kimkakati madini manne yako katika Mkoa wa Dodoma.
Meneja huyo alisema mkoa huo ni maarufu kwa upatikanaji wa miamba yenye madini ya lithium, chrysoprase, chuma, nikeli, urania na jasi.
Aidha, amesema taarifa hiyo imeonesha kuwa kuna madini ya yoderite yanayopatikana mlima wa Mautia wilayani Kongwa na imebainika kuwa madini hayo hadi sasa yanapatikana Tanzania pekee duniani kote.
Akipokea taarifa ya utafiti huo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema taarifa hiyo ni nyenzo itakayosaidia kutangaza mkoa wa Dodoma kimkakati husasan katika uwekezaji wa sekta ya madini.
“Nawashukuru sana GST kwa kuwasilisha kitabu hiki na ramani ya inayoonesha madini katika mkoa wa Dodoma, ni taarifa muhimu sana ya kuvutia wawekezaji kwa kuwa imeainisha aina ya madini na eneo yanapopatikana,” alisema mkuu wa mkoa.
Aidha, Senyamule pia ametoa wito kwa jamii kutumia taasisi hiyo ya Serikali katika kufanya utafiti wa ardhi kabla ya kuanza kwa ujenzi wa ghorofa katika ya 3-4 ili kuepuka madhara.
Sambamba na hayo ametoa rai kwa taasisi hiyo kushirikiana na Bonde la Wami Ruvu katika kuendeleza tafiti za wingi wa maji katika bonde hilo kwa kuwa taasisi ya GST imethibitisha kuwa na vifaa na utaalamu wa kutosha.