‘Down Syndrome si ugonjwa wa akili’
JAMII imeaswa kutambua kuwa down syndrome si ugonjwa wa akili, bali ni viungo kutokamilika na kufanya kuonekana kama wana mtindio wa ubongo, ilhali tatizo kubwa ni ubongo na moyo kuwa na tundu.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Down Syndrome, Mkurugenzi wa shirika hilo,Monyi Pettit, amesema watoto hao wanakuwa na misuli isiyo na nguvu hali inayosababisha kutokuwa vizuri, hivyo ni ugonjwa unaosababisha watoto wasikue vizuri.
Ametoa rai kwa jamii kutowanyanyapaa watoto hao au kuwaficha ndani, ikiwemo ukosefu wa elimu, kwani hivi sasa wanaishia elimu za msingi tu kupitia vitengo maalum, hivyo aliomba watoto hao nao wapewe vipaumbele zaidi katika elimu za sekondari.
Maadhimisho hayo hufanyika Machi 21 kila mwaka na yana kauli mbiu isemayo: “Pamoja nasi sio kwa niaba yetu.”
Aliomba takwimu za watoto hao zipatikane, ikiwemo elimu sahihi kwa jamii, ili wazazi na walezi wajue aina ya ulemavu huo, ikiwemo utambuzi wanapogundulika na tatizo hilo, ili waweze kupata huduma bora za afya.
Naye Mwenyekiti wa Shivyawata, Elisha Millya ,amesema bado walemavu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wengine kutumikishwa kuomba mitaani na wengine kutumikishwa na kunyimwa haki zao za msingi.
Amesisitiza Mkoa wa Arusha kuchukua hatua zaidi kudhibiti wimbi hilo kubwa la watoto wenye ulemavu kuomba.