CHANJO zaidi ya dozi milioni 60 kwa mwaka za ugonjwa wa mdondo ama kideri zijulikanazo kwa jina la kitaalam kama TEMEVAC, zinauzwa nchini Tanzania kwa wafugaji wa kuku hali inayochangia kuongeza kipato chao kwa kuwa hawashambuliwi na ugonjwa huo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dk Stella Bitanyi, amesema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLEO kuhusu ubora wa chanjo hiyo.
Akitaja kwa idadi ya kuku, Dk Bitanyi amesema dozi hiyo ikigawanywa waweza sema imehudumia kuku milioni 20 kwa maana kuwa kuku mmoja anapaswa kuchanjwa mara tatu kwa mwaka.
“Lakini dozi hiyo inaweza ikapanda kwa sababu kuna kuku waliochinjwa njiani wakaingia wengine hayo ni makadirio tu japo yanaweza kuwa zaidi,” amesema.
Amesema chanjo hiyo inazalishwa kwenye kituo chao cha chanjo kilichopo Kibaha Pwani, ambapo mpaka sasa kinazalisha chanjo za aina saba, ikiwemo chanjo hiyo pendwa dhidi ya mdondo.
“Chanjo hiyo ni ya kudhibiti mdondo wa kuku unaua sana ukiingia unaweza kukuta usibaki na kuku hata moja, pia imethibitishakuwa na uwezo mkubwa wa kuzuia mdondo hasa kwa kuku wa kienyeji ni chanjo ya maji maji inawekwa kama matone.
“Chanjo hiyo ina uhakika wa asilimia 100 ya kumkinga kuku dhidi ya mdondo,” amesema.
Naye Meneja wa Kiwanda cha Chanjo Tanzania kiichopo chini ya wakala huo, Charles Mayenga amesema wakati taasisi hiyo inaanzishwa ilianza kwa kuzalisha chanjo hiyo ya mdondo.
Amesema walianza kwa kuzalisha chanjo hiyo ya dozi 400 ikapunguza ikawa na dozi 200 na kwamba chanjo hiyo ina uwezo wa kukaa kwenye friji kwa miezi minne.
“Tumeendelea kuwapelekea chanjo wafugaji wakaomba wapunguze dozi wakatengeneza chanjo ya dozi 50,” amesema