UWEKEZAJI utakaofanywa na Kampuni ya DP World (DPW) ya Dubai katika Bandari ya Dar es Salaam utapunguza gharama za bidhaa kwa wananchi zinazoagizwa kutoka nje kupitia bandari hiyo kutokana na teknolojia itakayotumika kuharakisha upakuaji na upakiaji wa mizigo bandarini hapo.
Moja ya sababu inayochangia bidhaa kuwa ghali kwa sasa ni ucheleweshaji wa meli kuingia bandarini kutoka nangani au eneo zinakoegeshwa kusubiri kuingia bandarini hali inayofanya wakala wa mzigo huo kulipa tozo kubwa kwa mwenye meli.
Akizungumza na HabariLEO ofisini kwake, Mkuu wa Chuo cha Bandari, Dk Hussein Lufunyo alisema meli inaposubiri nje ya bandari hulipwa Dola za Marekani 25,000 ambayo ni takribai Sh milioni 60 kwa siku.
Dk Lufunyo alisema gharama hiyo ya Dola 25,000 inalipwa na wakala aliyeagiza mzigo huo hali itakayomlazimu mfanyabiashara wa mzigo huo naye kupandisha bei ya bidhaa zake sokoni na kumfanya mwananchi ambaye ni mtumiaji wa mwisho kulazimika kulipia gharama hiyo kwa kuinunua bidhaa kwa bei kubwa.
“Mtu anapopakia mzigo China au Malaysia, kwenye gharama zake anaongeza na gharama za meli kukaa nangani, maana yake mzigo unaoletwa kwenye bandari yetu ni wa gharama kubwa, kwa mfano unaagiza gari aina ya Toyota na unatakiwa kulipa Dola 2,000 kama malipo ya kusafirishia, lakini utajikuta unalipa Dola 2,500, kama ufanisi wa bandari ungekuwa mzuri gharama ingekuwa ndogo,”alisema Dk Lufunyo
Alisema Bandari ya Dar es Salaam ina changamoto mbalimbali ikiwemo muda wa meli kusubiri nangani na muda wa meli kukaa gatini.
Dk Lufunyo alisema meli kukaa muda mrefu nangani inasababishwa na uchache wa magati na uhaba wa vifaa vya kupakia na kushusha mizigo kwenye meli, hivyo kama kungekuwepo vifaa vya kisasa na vya kutosha kungesaidia kupakua meli kwa haraka na kuondoka ili kuruhusu meli nyingine kutia nanga gatini.
”Kwa kuwa sisi tuna vifaa vichache na magati machache, ndiyo maana meli nyingi utazikuta zimetia nanga nje ya bandari, sisi tuna magati takribani 12, lakini washindani wetu kama Bandari ya Mombasa wana magati 26 mpaka 30, maana yake wao kwa wakati mmoja wana meli 26 au 30 zinapakuliwa gatini,”alisema
Dk Lufunyo alisema takwimu zinaonesha kuwa muda wa meli kukaa nangani kusubiri kuingia gatini katika Bandari ya Mombasa ni wastani wa siku 1.2 lakini katika Bandari ya Dar es Salaam kwa wakati mmoja kunaweza kuwa na meli 11 au 12 gatini, hivyo meli moja inaweza kuchukua siku tatu hadi sita kupakuliwa kutegemeana na mzigo uliopo.
Alisema wakati meli moja inachukua hadi siku sita kupakuliwa gatini maana yake kuna meli nyingine inasubiri nangani kwa wastani wa siku hizo hizo sita au zaidi kuingia gatini kwa kuwa muda wa kusubiri nangani unahusiana na muda wa gatini hali inayofanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa ya gharama ikilinganishwa na bandari za nchi jirani kama Bandari ya Durban ambako meli huchukua siku 1.6 kukaa gatini.
Jambo jingine linalofanya huduma za Bandari ya Dar es Salaam kuwa juu ni ufanisi mdogo gatini kutokana na vifaa, teknolojia na weledi au maarifa ya uendeshaji.
Pia alisema kutokuwepo kwa maegesho ya kutosha katika eneo hilo la bandari ni changamoto nyingine inayohitaji kampuni kubwa yenye uwezo kama DPW kuwekeza bandarini hapo.
Dk Lufunyo alisema ufinyu wa maegesho unasababisha kuwepo kwa msongamano wa mizigo na kufanya uendeshaji wa mitambo ya kubebea mizigo kama forklift au winchi kutumia muda mrefu kutoa mzigo sehemu moja kwenda nyingine kwa hofu ya kudondokewa na mizigo hiyo.
Kutokana na changamoto zote hizo ambazo zinachangia Bandari ya Dar es Salaam kukimbiwa na wateja, alisema serikali imeona vyema kupata mwekezaji kama DP World yenye uwezo wa vifaa, teknolojia, mifumo na uzoefu wa masuala ya uendelezaji na uendeshaji wa bandari duniani.
Dk Lufunyo alisema DP World inashika nafasi ya tano kati ya waendeshaji wakubwa wa bandari duniani na inahudumia takribani asilimia tisa ya shehena yote ya makasha inayosafirishwa duniani.
Alisema kampuni hiyo inaendesha bandari 190 duniani katika nchi 68 zilizopo ndani ya mabara sita ya dunia, pia inatoa huduma za bandari kwenye nchi zaidi ya 70 ikiwemo China, Saudi Arabia, Korea, Uingereza, Australia, Chile, Ufaransa, Vietnam, Canada, Pakistani, Ubelgiji, India, Indonesia, Argentina na Brazil.
Pia alisema DP World ina uzoefu wa zaidi ya miaka 20 Afrika katika uendeshaji wa bandari hususani katika nchi sita ikiwemo Senegal katika Mji wa Dakar, Algeria (Aligiers, Djen Djen), Angola (Luanda), Kigali nchini Rwanda na Maputo nchini Msumbiji.
Comments are closed.