CHUO cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA) kimeendelea kutoa elimu na mafunzo mbalimbali kwa maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali katika kukabiliana na majanga ya moto.
Akitoa taarifa hiyo leo Mei 30, 2023 Mkuu wa DPA, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Dk Lazaro Mambosasa amesema chuo hicho kimekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa wanafunzi wa kozi mbalimbali.
Alisema lengo kubwa la kutoa mafunzo hayo ni kujenga uwezo kwa maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali wa Jeshi hilo na makundi mengine ya wahitaji.
Aidha alielezea umuhimu wa kila askari kuwa na vifaa wezeshi ili kukabiliana na majanga pindi yanapotokea.
Pia SACP Dk Mambosasa alitumia fursa hiyo kumpa pole mkufunzi wa chuoni hapo aliyepata majanga ya kuunguliwa moto nyumba yake.
Kwa upande wake Sajenti Saidi Hamad aliyepata janga hilo la kuunguliwa moto nyumba yake aliushukuru uongozi wa chuo kwa namna walivyoguswa na kumuonesha ushurikiano huku akisema japo nyumba yake yote iliungua lakini familia iko salama.