KAMPUNI ya DPO Pay inayotoa huduma za malipo ya kidijitali imetambuliwa na kupewa kibali na Benki Kuu ya Tanzania kuendesha huduma zake.
DPO Pay yenye makao makuu yake nchini Kenya, itaendeleza shughuli zake nchini baada ya kuwa imetambuliwa kwa mujibu wa sheria na kupata leseni.
Tumefurahi kupokea leseni hii kutoka kwa Benki Kuu ya Tanzania. Kwa kuzingatia dhamira yetu thabiti yakuongeza wigo wa utoaji huduma zetu katika nchi za Afrika Mashariki, kibali hiki ni sehemu yakuonesha nia yetu na uthabiti wetu wa kufuata taratibu zote za kisheria na kiutaratibu katika kuendesha shughuli zetu nchini Tanzania.” Mkurugenzi Mtendaji wa DPO Pay, Judy Waruiru alisema.
DPO Pay ambayo sasa ipo chini ya shirika la Network International, shirika ambalo ni wezeshaji mkuu wa biashara za kidigitali katika eneo la Afrika Mashariki na Kati iko tayari kutoa huduma zake nchini Tanzania.
Judy amebainisha utayari wa DPO Pay katika kuchagiza na kuwezesha ujumuishaji kifedha kwa makundi mbalimbali na ustawi wa biashara kidigitali.
Mifumo ya DPO ni thabiti na inahakikishia watumiaji wake kama wafanyabiashara kuweza kufanya miamala kwa urahisi, ufanisi, uhakika na haraka zaidi huku ikihakikishia watumiaji wake ulinzi wa taarifa zao.
“DPO Pay ina mifumo thabiti inayohakikisha ulinzi wa taarifa za mtumiaji na ubora wa huduma. Kwa kutumia DPO Pay Mobile inayopatikana (istore/playstore), wateja wetu wanauhakika wakupata huduma mbalimbal katika ubora na upekee,” alisisitiza Judy.
DPO Pay tayari inafanyakazi Zanzibar na kutumiwa na wafanyabiashara wa hoteli, usafiri na watu binafsi kuupokea na kufanya malipo kupitia DPO Pay.
Huduma za DPO Pay zinatoa fursa kubwa kwa wafanyabiashara, na watu binafsi kuendesha malipo kidigitali ndani na nje ya nchi. Kwa sasa DPO Pay inaendesha shughuli zake katika nchi 20 barani Afrika. Pia kupitia DPO Pay, mteja anaweza kufanya malipo kupitia kadi ya benki, simu, kuhamisha fedha n.k.