DPP: Sabaya sasa yupo huru
ARUSHA: MKURUGENZI wa Mashtaka Nchini (DPP), ameondoa Rufaa yake katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha dhidi ya kesi ya uhujumu uchumi namba 27 iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita.
Katika rufani hiyo, waleta rufani alikuwa DPP na wajibu rufani ni Sabaya akiwakilishwa na Wakili Mwandamizi Jijini Arusha, Moses Mahuna na washtakiwa wengine akiwemo Silvester Nyegu (26), Enock Togolani (41), John Odemba, Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31).
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya viwanja vya Mahakama, Wakili Mahuna, alieleza kuwa “Baada ya Mahakama ya Rufani ya Tanzani kufanya marejeo na mapitio ya namna shauri lilivyokuwa likiendeshwa iliamua kufuta mwenendo mzima na kuamua rufani hii kuanza kusikilizawa upya.
“Leo Rufani hii imeitwa kwa ajili ya kusikilizwa baada ya uamuzi ule wa Mahakama ya Rufani wa kubatilisha mwenendo ambao ulikuwa umeanza kusikiliza awali,” alieleza Mahuna.
Wakili Mahuna, alieleza Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa serikali, Akisa Mhando aliwasilisha taarifa ya DPP na kusema kuwa DPP hana nia ya kuendelea na rufani na kuamua kuiondoa katika mahakama hiyo.
“Mahakama baada ya kupokea notisi ya DPP imefuta rufani hii rasmi leo mbele ya Mahakama Kuu hivyo Sabaya hana tena kesi inayomkabili kwa kuwa zote zimekwisha malizika,” alieleza Mahuna.