MSHEREHESHAJI na muigizaji maarufu nchini, Mahsein Awadhi ‘Dr Cheni’ amesema kuwa sio kweli kwamba alishindwa kufanya kazi ya harusi ya Jacqueline Wolper na mumewe Rich Mitindo sababu ya pesa.
Alisema kuwa watu wamekuwa wakiongea vitu wasivyokuwa na uhakika navyo, kwani wakati anaongea na Jacqueline kuhusu kufanya kazi kwenye harusi yao tayari alikuwa na kazi nyingine mkononi, hivyo ikawa ngumu.
“Kuhusu kushindwana kwenye kiasi cha pesa sio kweli kazi ziliingiliana na ile ya watoto wanne wa mmiliki wa mabasi ya Kilimanjaro, hivyo sikuwa na njia nyingine ya kufanya kazi,”
“Sisi washereheshaji huwa tunafanya kazi kwa ratiba ili kuepusha kazi kuingiliana, hivyo ndivyo ilivyotokea japokuwa nilitamani kufanya kazi hiyo kutokana na maelewano mazuri tuliyokuwa nayo,” alisema Dr Cheni.
Alisema kuwa watu wanapaswa kuangalia maneno wanayoongea juu ya kazi ya mtu mwingine kwani kila mtu ana uwezo wake wa kutafsiri kilichoongelewa na mwisho kazi yake ni kusherehesha hawezi kuacha kazi inayomuingizia fedha.