Dr Mpango aongoza kumuaga Mrema

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema aliyekuwa Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema alikuwa ni kiongozi mkweli na mzalendo kwa taifa na wakati wote alitetea maslahi ya nchi.

Dk Mpango alisema hayo jumatano asubuhi wakati yeye na mkewe, Mama Mbonimpaye walipokwenda nyumbani kwa Mrema Salasala jijini Dar es Salaam kutoa pole kutokana na kifo cha kiongozi huyo.

Mrema aliaga dunia Agosti 21 asubuhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dar es Salaam.

Akiwa nyumbani kwa Mrema, Dk Mpango aliwapa pole wana familia akiwemo mjane wa Mrema, Doreen Mrema, viongozi wa TLP na akawaomba wawe na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu.

Akiwa na waombolezaji wengine, Dk Mpango na mkewe waliongoza sala ya kumuombea Mrema. Dk Mpango alisema taifa limepoteza kiongozi aliyetumikia vizuri nafasi alizowahi kuongoza katika uhai wake.

Mrema aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Naibu Waziri Mkuu, Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Mbunge wa Temeke (NCCR-Mageuzi), Mbunge wa Vunjo (TLP) na hadi anafariki dunia alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana alisema serikali itaendelea kumkumbuka Mrema kutokana na mchango wake kuendeleza uhusiano na vyama vya siasa. Majaliwa alisema hayo jumatano mchana alipozungumza na mamia ya waombolezaji kwenye ibada ya kumuaga Mrema katika Parokia ya Mtakatifu Augustino Kilimahewa, Salasala, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

“Mheshimiwa Mrema atakumbukwa kama kiongozi mkuu wa Chama cha TLP kwa muda mrefu sana. Na akiwa katika siasa, aliisaidia serikali kupata mwelekeo mzuri wa vyama vya siasa,” alisema na akabainisha kuwa salamu za Rais Samia Suluhu Hassan ziliwasilishwa na Dk Mpango.

Aliongeza: “Sisi tuliopo hapa tuna mambo mawili makubwa ya kufanya ili kumuenzi ndugu yetu Mrema. Moja ni kuenzi yale yote aliyofanya kwa upande wa serikali na upande wa siasa.” Majaliwa alisema leo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni wataiwakilisha serikali katika maziko ya Mrema Kiraracha, Moshi.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Henry Mchamungu alisema umati uliokuwa kanisani hapo ni ishara ya namna Mrema alivyoishi na watu wakiwemo viongozi wa serikali na vyama vya siasa.

Paroko wa kanisa hilo, Padri Peter Assenga alisema Mrema alikuwa akijitolea kwa mambo mengi parokiani hapo na ataendelea kukumbukwa sana.

Ibada hiyo iliongozwa na Askofu mmoja na mapadri sita. Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Profesa Ibrahim Lipumba, John Cheyo, Stephen Wasira na James Mbatia.

Mrema ameacha mjane, Doreen na watoto watano wakiwemo wanne wa kike na mmoja wa kiume.

Habari Zifananazo

Back to top button