Dr Mpango aonya biashara ya ‘unga’, uvuvi haramu

SERIKALI imeonya wanaojihusisha na uhalifu mkoani Tanga ikiwamo biashara haramu ya dawa za kulevya, biashara za magendo, uvuvi haramu, wahamiaji haramu na biashara ya binadamu.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alitoa onyo hilo jana alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa gati mbili na uongezaji kina kutoka meta tatu hadi meta 13 unaondelea katika Bandari ya Tanga.

Aliagiza viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi washirikiane kutatua changamoto za uhalifu na watakaojihusisha watajwe ili waondolewe.

Advertisement

Alimuagiza alimuagiza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) atupie jicho Tanga kudhibiti upotevu wa mapato na kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato.

Aidha, aliagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ihakikishe miradi yote ya maboresho ya bandari ya Tanga inakamilika ifikapo Aprili mwakani.

Miradi ya maboresho ya Bandari ya Tanga inagharimu Sh bilioni 429 na inatarajiwa kuongeza ufanisi kufikia kuhudumia tani milioni tatu kwa mwaka kutoka tani 750,000 za sasa.

Alisisitiza kuwa ni lazima bandari hiyo ifanye kazi kwa viwango na kuvutia zaidi watumiaji wa bandari katika Afrika Mashariki.

Alimuagiza Meneja wa Bandari ya Tanga kushughulikia haraka malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu utendaji wa bandari hiyo ikiwamo utoaji mizigo kutumia muda mrefu.

Dk Mpango alisema upungufu katika bandari ya Tanga umesababisha wafanyabishara watumie bandari za nchi jirani na hivyo kukosesha taifa mapato.

Aliiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutoa ushirikiano kufanikisha uchunguzi unaoendelea wa ghala la forodha la TRA Tanga kuungua moto.

Aidha, alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba kusimamia wote wanaopaswa kujibu hoja zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhakikisha wanazijibu haraka ili kukabiliana na ubadhirifu wa fedha za umma.