DRC wamfukuzisha Mreno Misri

CAIRO, Misri: SHIRIKISHO la Mpira wa miguu nchini Misri (EFA) limefuta kibarua cha Kocha wa timu ya taifa ‘The pharaoh’ Rui Vitoria (53).
Taarifa kutoka EFA zinaeleza kuwa kandarasi yao na Vitoria ilipaswa kudumu hadi Kombe la Dunia la 2026 lakini safari ya mapema ya Mreno huyo imechagizwa na kufurushwa katika hatua ya 16 bora ya Fainali za 34 za Mataifa Afrika (AFCON 2023) nchini Ivory Coast.
Katika hatua hiyo, Misri ilikabiliana dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa penalti 7-8 baada ya dakika 120 kuhitimishwa kwa sare ya 1-1.
EFA imesema si tu kocha huyo amesitishiwa kandarasi ila wasaidizi wake pia wamejumuishwa katika mkumbo huo huo.
Aidha, imemtangaza Mohamed Youssef, kocha wa zamani wa Al Ahly ambaye
aliwaongoza wababe hao wa Misri kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL 2013) kukaimu nafasi hiyo kwa muda.
“Shirikisho pia litasoma ‘CV’ wasifu wa makocha kadhaa, baadhi yao wakiwa ni wakigeni,” EFA imeeleza katika taarifa yake.
Vitoria alitawazwa kuwa bosi wa Misri mwaka 2022, akirithi timu iliyokosa ubingwa wa AFCON majuma kadhaa baada ya kupoteza fainali dhidi ya Senegal kwa matokeo ya penalti 2-4 katika ardhi ya Cameroon.