‘Drone’ yarushwa utafiti wa miamba, madini

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde ameshuhudia jaribio la urushwaji wa ndege nyuki ‘Drone’ angani kwa ajili ya utafiti wa miamba na madini lililofanyika katika kijiji cha Utimbe kata ya Lupaso wilayani Masasi mkoani Mtwara.

Akizunguza katika eneo hilo la utafiti wa madini hususani kinywe, bati, shaba, na chuma, waziri huyo amesema mpaka sasa Tanzania ina taarifa za kina za tafiti wa miamba na madini kwa asilimia 16 zilizopelekea uwepo wa migodi mikubwa ya kati na midogo.

‘’Nchi ikifanyiwa utafiti wa kina wa high resolution airborne geophysical survey wa angalau asilimia 50 ifikapo 2030  itasaidia ongezeko kubwa la uwekezaji katika sekta ya madini.’’amesema Mavunde

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kwa dhati kuhakikisha inawasaidia wachimbaji wadogo wa madini kwa kuwapatia maeneo yenye taarifa za jiolojia ili wachimbe kwa faida na kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na na Utafiti wa Madini nchini (GST) Dk Mussa Budeba amemshukuru waziri huyo kwa kukubali kushiriki na kushuhudia jaribio hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas, ameipongeza wizara hiyo kwa kurusha ndege  hiyo kwa ajili ya utafiti katika eneo lake na kuiomba kusaidia upatikanaji wa soko la madini ya chumvi na kujengwa kiwanda cha kuchakata madini hayo mkoani humo.

Katibu Mkuu wa Chama cha wachimbaji madini mkoani humo Abdallah Ally ‘’zoezi hili tumelipokea kwa furaha sana ni swala ambalo tulikuwa tunalitafuta kwa siku nyingi, siku zote tulikuwa tunachimba lakini kwa kubahatisha, linapotokea hili tuna uhakika uchimbaji sasa mtwara utakuwa kama iliyokuwa mikoa mingine kama vile Kahama na mingine’’

Aidha, mpaka sasa majaribio ya utafiti huo unaoendelea kufanyika mkoani Mtwara, tayari umefanyika kwenye mkoa ya Dodoma, Shinyanga, Geita, Manyara na Lindi.

Katika zoezi hilo, GST imeshirikiana na kampuni zingine ndani na nje nchi ikiwemo ya Tuku Tech Kampani Ltd kutoka hapa nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button