Dua ya Ijitimai kuanza leo Mpanda

WAUMINI wa dini ya Kiislamu kutoka mataifa mbalimbali wameanza kuwasili mkoani Katavi katika ibada ya siku tatu ya Ijitimai ya kimataifa inayoanza leo ikilenga kuendeleza amani na utulivu.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Shehe wa Mkoa wa Katavi, Mashaka Kakulukulu alisema Ijitimai ni ibada inayokusanya waumini wa dini hiyo kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujengana kiimani na pia kufanya dua mbalimbali.

Shehe Kakulukulu alisema kufanyika kwa ibada hii mkoani Katavi ni fursa ya kutangaza mkoa, wafanyabiashara kujiingizia kipato. Mkutano huo unaanza leo katika viwanja vya Shule ya Sekondari Istiqama mjini Mpanda.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Ijitimai ya Kimataifa, Hassan Mwinyi alisema wageni takribani 2,000 kutoka mataifa mbalimbali wanatarajia kuhudhuria. Aliwasihi waumini wote kujitokeza ili kwa pamoja waweze kumwomba Mungu kwa kila mmoja kadri ya uhitaji wake.

Baadhi ya washiriki ambao wamewasili mkoani Katavi kutoka Zanzibar akiwemo Hafidh Jabu, walieleza kufurahishwa na mapokezi mazuri waliyopata.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button