Dubai waadhimisha Siku ya Mtanzania
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Selemani Jafo ameshiriki hafla maalum ya Maadhimisho ya Miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania, Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) iliyotambulika kama Siku ya Mtanzania kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Waziri Jafo amesema Serikali inatambua mchango na umuhimu wa Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) katika kuleta maendeleo nchini Tanzania.
Waziri Jafo Amesema tayari Serikali imechukua hatua hatua ya kusaini Hati ya Makubaliano ya ushirikiano kwenye kazi na ajira uliosainiwa katika kipindi cha Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) unaoendelea.
Huku akisaema hatua hiyo itasaidia katika kutatua changamoto nyingi zilizokuwepo za wafanyakazi hasa wa majumbani na wote kwa ujumla watakuwa katika mazingira mazuri ya kisheria kwa pande zote mbili.
Waziri Jafo amesema hatua hizo za makusudi ni mojawapo ya mikakati ya Serikali katika kuhakikisha Diaspora wanawekewa mazingira wezeshi ya kuwatambua kisera na hatimae kisheria.
“Ni mategemeo ya Serikali kuwa Diaspora mtakuwa na upendeleo maalumu ikiwa ni pamoja na kuweza kurudi Tanzania kirahisi na kuweza kunufaika na fursa mbalimbali za kichumi tofauti na wageni kwani katika kipindi chote cha historia, uhusiano kati ya Tanzania na UAE umekuwa wa kipekee,“ amesema Dk.
Jafo.
Aidha, Dk. Jafo ameongeza kuwa yapo mafanikio mengi yakiwemo ushirikiano wa kibiashara, utamaduni na maendeleo ya kijamii na ili kuendelea kunufaika na fursa zilizopo katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kupitia uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi mbili.
Kwa upande mwingine amesema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imezindua mfumo wa mawasiliano na Diaspora wake kote duniani uitwao Diaspora Digital Hub System (DDH) ambao utasaidia usajili wa wanadiaspora wa makundi yote kwa lengo la kuwatambua na kuwaweka katika mfumo maalum ili iwe rahisi kwa mawasiliano na kuwaunganisha katika mitandao ya huduma muhimu.