MWIGIZAJI Kulwa Kikumba ‘Dude’ amesema amesikitishwa na kitendo cha mwanamuziki wa singeli, Dulla Makabila kumzushia kifo jana kitendo ambacho kiliwashtua wengi.
Makabila alitoa tangazo la kifo cha Dude jana ikiwa ni siku ya wajinga duniani kitendo ambacho kwa wale ambao hawakujua waliamini na wale waliojua walipuuza na wengine wakihamaki na kutukana.
Baada ya Dude kuhojiwa jana alisema alishangazwa na taarifa hizo kwani msanii mwenzake, Jacqueline Wolper alimpigia simu na kuanza kulia kuhusu kifo chake.
“Mimi imenishangaza, Jacqueline Wolper alinipigia simu huku analia kuniambia mbona nimetangazwa kuwa nimekufa. Sio yeye tu bali kulikuwa na simu nyingi sikupokea nikajua wanataka kuniuliza jambo hilo,” alisema.
Dude alisema alijaribu kumpigia Makabila kuzungumza naye jambo hilo lakini hakupokea simu.
Alisema kitendo hicho kitawaathiri wengi lakini zaidi msanii mwenyewe aliyetoa taarifa za uongo kwa sababu atapoteza imani kwa mashabiki zake waliokuwa wanamwamini.
“Waniombee amani, sijajisikia vizuri kwa kweli, vitu kama hivi vitawafanya watu waache kukuamini kwa upuuzi,” alisema.