DUWASA yafanya kweli maji Nzuguni

DUWASA yafanya kweli maji Nzuguni

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), inaendelea na uchimbaji wa visima na tayari imechimba visima vitano katika Kata ya Nzuguni, mkoani Dodoma.

Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, wakati wa ziara ya Mbunge wa Dodoma Mjini, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde, aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri waliokuwa wakifuatilia hatua zinazochukuliwa na mamlaka hiyo katika kutatua changamoto ya maji mjini Dodoma.

Mhandisi Aron amesema kuwa zaidi ya wakazi 37,000, waishio katika ukanda wa Nzuguni jijini Dodoma, wanatarajia kunufaika na mradi wa maji, baada ya kubainika uwepo wa bonde lenye maji mengi katika eneo hilo.

Advertisement

Amesema kukamilika kwa mradi huo, kutaongeza uzalishaji wa majisafi kutoka wastani wa lita milioni 67.8 hadi lita milioni 75.5 kwa siku, sawa na ongezeko la asilimia 11.4 ya uzalishaji wa sasa.

Kwa upande wake Mavunde, ameipongeza DUWASA kwa kuweza kushirikiana na wananchi katika kutatua kero ya maji licha ya changamoto zote zilizopo.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Jabir Shekimweri ameshauri wananchi wanaopisha miradi hiyo kulipwa fedha zao mapema, ili eneo libaki kuwa chanzo cha maji na wanaojenga wajulishwe kuhusu kuzingatia suala la upandaji miti ili kutunza mazingira.