EABC kukutanisha vigogo wa biashara Afrika Mashariki

BARAZA la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) kwa kushirikiana na Afreximbank linaandaa mkutano wa Wakuu wa Biashara na Uwekezaji wa Afrika Mashariki 2023 utakaofanyika nchini Uganda.
Mkutano huo wenye kaulimbiu: ‘Ushirikiano wa Kikanda Unaoendeshwa na Sekta Binafsi kwa Ajili ya Kuongezeka kwa Biashara ya Ndani ya Afrika, Uwekezaji na Ukuaji wa Uchumi’, umepangwa kufanyika Agosti 31 hadi Septemba Mosi, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa EABC, John Bosco Kalisa mkutano huo utajadili mafanikio na vikwazo vya biashara na uwekezaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).
Kalisa alisema mkutano huo unaotarajiwa kukutanisha zaidi ya wajumbe 500 wakiwamo mawaziri, maofisa wakuu wa serikali, wakuu wa sekta, wawekezaji watarajiwa na taasisi za kifedha watajadili na kushirikishana maendeleo na maarifa.
“Mkutano huu umeandaliwa kwa ushirikiano wa karibu na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, sekta binafsi Uganda, Uganda Manufacturers Association na Uganda Investment Authority.” “Mkutano utaonesha mwelekeo wa siku zijazo na mageuzi ya sera yanayohitajika ili kuleta mafanikio ya haraka katika kuongeza viwango vya juu vya uwekezaji na biashara katika EAC na Afrika kwa ujumla,” alisema.
Akaongeza: “Mamlaka zote za kukuza uwekezaji katika EAC zitaonesha fursa na kuwasilisha miradi inayowezekana tayari kwa uwekezaji kwa wawekezaji wa Afrika Mashariki, Afrika na kimataifa.” Kalisa alisema washiriki watajadili mwelekeo na mabadiliko ya mazingira ya kiuchumi duniani pamoja na katika Bara la Afrika na hatimaye, kuweka upya EAC kama eneo bora zaidi la uwekezaji barani Afrika. Aidha, alisema washiriki watajadili hali ya biashara na uwekezaji na namna ya kuifanya Afrika Mashariki kuwa eneo linaloongoza la biashara na uwekezaji.