EABC yazindua utafiti fursa za uwekezaji EAC

BARAZA la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) chini ya Mfuko wa Skauti wa Biashara na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ), limezindua utafiti unaobainisha fursa za uwekezaji katika minyororo ya thamani ya kilimo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mkurugenzi Mtendaji wa EABC, John Bosco Kalisa alisema utafiti huo unalenga kushughulikia uwekezaji wa moja kwa moja katika kilimo na ustahimilivu wa chakula kutoka nje.

“Matokeo ya utafiti yatawezesha kuorodhesha fursa za uwekezaji zilizochaguliwa katika mnyororo wa thamani wa EAC,” alisema.

Alisema utafiti utaonesha uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni katika eneo la EAC uliongezeka kidogo kati ya mwaka 2015 na 2021 hasa kutokana na uwekezaji kutoka China na India hususani katika viwanda, ujenzi na sekta ya huduma.

Alisema mradi wa GIZ Business Scout Fund – EABC unalenga kuimarisha ushindani katika sekta ya chakula na kupunguza athari za migogoro ya kimataifa ili kuboresha usalama wa chakula EAC.

Alisema mtandao huo uliwakutanisha watoa uamuzi wa ngazi za juu wa sera na zaidi ya watendaji 60 wa mnyororo wa thamani katika kilimo.

Kalisa alisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi katika utendaji wa sekta ya kilimo ili kukuza biashara na uwekezaji wa ndani ya kikanda.

Alisema ipo haja ya kuchukuliwa hatua za makusudi kujenga ustahimilivu wa kilimo nchini ili kukabiliana na migogoro ya kimataifa.

Alipendekeza matumizi ya mchanganyiko wa sera ili kutoa bima ya kilimo na kuendeleza hifadhi.

Mwakilishi wa GIZ Business Scouts for Maendeleo, Michael Kleinbub alipongeza juhudi za jumuiya ya wafanyabiashara kushughulikia chakula na masuala ya usalama.

Aliahidi msaada wa Skauti za Biashara kwa Maendeleo nchini ili kuwezesha ushirikiano kupitia programu na ubia kati ya sekta ya umma na binafsi sambamba na kutoa msaada wa kifedha na kiufundi kwa kampuni zinazowekeza katika uendelevu wa masoko.

Kwa mujibu wa Kalisa, utafiti unaonesha kuwapo uwezekano mkubwa wa kuendeleza minyororo ya thamani katika ngano, mafuta ya kula, mbolea, mizizi na mimea ya kunde ndani ya EAC.

Habari Zifananazo

Back to top button