EAC yapewa ushauri mpya kuhusu DRC

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imeshauriwa kuyashirikisha mataifa yenye nguvu duniani katika kutafuta amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kuwa mataifa hayo yana ushawishi mkubwa katika kanda hiyo.

Wataalamu na wachambuzi wa diplomasia na uchumi nchini wameliambia HabariLEO Afrika Mashariki jana kuwa mataifa hayo makubwa ndiyo yaliyosaidia kufikia suluhisho katika mgogoro kati ya Serikali ya Ethiopia na waasi wa Tigray na kuhitimisha vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mchambuzi wa masuala ya diplomasia, Profesa Humphrey Moshi alisema mataifa makubwa ndiyo yaliyosaidia kufikiwa kwa suluhu katika mgogoro wa Ethiopia baada ya juhudi za muda mrefu za Umoja wa Afrika (AU) kushindwa kumaliza vita hiyo.

Alisema pamoja na mazungumzo kupewa kipaumbele kati ya pande zinazohusika, EAC haina budi kutumia pia mbinu za kushirikisha mataifa makubwa ambayo pia yana uwezo wa kuzuia uingizaji wa silaha zinazowafikia waasi na kuleta madhara kwa wananchi wa DRC.

“Asilimia kubwa ya mafanikio ya migogoro duniani ilishirikisha mataifa makubwa katika utatuzi wake, mfano ni waasi wa UNITA waliisumbua sana Serikali ya Angola, lakini yaliposhirikishwa mataifa makubwa katika kutafuta suluhu, mgogoro ule ulimalizika,” alisema Profesa Moshi.

Mchambuzi mwingine wa masuala ya uchumi na siasa, Gabriel Mwang’onda alisema kwa kuwa njia za kusaka amani zinaendelea kutumika, kabla ya matumizi ya nguvu za kijeshi yashirikishwe mataifa makubwa ambayo yana ushawishi DRC.

Alisema matumizi ya nguvu za kijeshi hayajawahi kuzaa matunda yanayohitajika. Mwang’onda alitoa mfano wa Somalia ambako kumekuwa na matumizi makubwa ya nguvu za kijeshi yakiongozwa na Marekani, Kenya na wakati fulani Ethiopia iliyoivamia Somalia kupambana na Al Shabaab, lakini hadi leo bado kundi hilo ni tishio nchini humo.

“Naamini pamoja na nia nzuri ya viongozi wetu wa EAC kutaka kuleta amani ya kudumu DRC, kabla ya kutumia nguvu za kijeshi wanatakiwa kujumuisha mataifa makubwa katika mchakato wa kutafuta amani kwa sababu waasi watakavyozungumza na wasuluhishi wa EAC, ni tofauti na watakavyozungumza na mataifa makubwa,” alisema.

Mtaalamu wa diplomasia, Profesa Kitojo Wetengere, alisema kabla ya matumizi ya nguvu dhidi ya waasi waliokataa kutii makubaliano ya Luanda, EAC ilitakiwa kuendelea kuzungumza na waasi kwa kushirikisha mataifa makubwa kama waangalizi na washauri.

Hivi karibuni, DRC ilifikia makubaliano na Rwanda kuwataka waasi wa M23 na makundi mengine ya waasi walioko Mashariki mwa nchi hiyo kuweka silaha chini na kuondoka katika maeneo wanayoshikilia hadi kufikia Ijumaa jioni wiki iliyopita.

Habari Zifananazo

Back to top button