EAC yataja vipaumbele 10 vya bajeti EALA

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imetaja vipaumbele 10 vya Bunge la Afrika Mashariki (EALA) katika kipindi cha Mwaka wa Fedha wa 2023/24 ikiwamo kuandaa Ofisi ya 16 ya Spika wa EAC mjini Juba nchini Sudan Kusini na kuandaa Mpango Mkakati wa 4 wa Bunge (2024 -2029).

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Afrika Mashariki, Vijana, Michezo na Utamaduni wa Burundi, Dk Ezechiel Nibigira alibainisha hayo wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya EAC kwa Mwaka wa Fedha wa 2023/24.

Katika uwasilishaji wake mbele ya EALA, Nibigira alisema Bunge la Afrika Mashariki limetengewa bajeti ya Dola za Marekani, 17,681,365 (takribani Sh 42,448,519,378/40 za Tanzania).

Alitaja kipaumbele cha kwanza kuwa ni kupitishwa kwa miswada iliyosalia ambayo ni sharti la kuanzishwa kwa Muungano wa Fedha pamoja na kutunga miswada inayosubiri kutoka katika Bunge la 4 ambayo ni Muswada wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu (PWDs) na Muswada wa Sheria ya Vijana wa EAC.

Kwa mujibu wa Nibigira, mingine ni Muswada wa Sheria ya Biashara ya Mipaka ya EAC katika Huduma za Kitaalamu; Muswada wa Sheria ya Dawa za EAC, Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Nembo za EAC; Muswada wa Sheria ya Afya ya Ujinsia na Uzazi wa EAC; Muswada wa Sheria ya Urithi wa Utamaduni wa EAC pamoja na Muswada wa Sheria ya Tathmini ya Usanifu, Ithibati na Ulinganifu wa EAC. Hotuba ya bejeti ilitaja vipaumbele vingine katika bajeti ya EALA kuwa ni pamoja na kuimarisha kazi ya uangalizi ya Bunge ili kuhakikisha kuwa Waafrika Mashariki wananufaika kikamilifu kutokana na utekelezaji kamili wa itifaki ya soko la pamoja na kuimarisha ushirikiano wa Bunge na mabunge ya kitaifa ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika utangamano kupitia wawakilishi wao.

“Vipaumbele vingine ni kuharakisha utekelezaji na uendeshaji wa mamlaka ya Bunge ya kiutawala na kifedha; kurekebisha Kanuni na Taratibu za EALA; kuandaa na kuwasilisha mapendekezo ya kurekebisha Mkataba wa EAC; kukagua utekelezaji wa maazimio na mapendekezo ya Bunge na kujenga uwezo kwa Wajumbe wa Bunge la 5 na wafanyakazi ili kutekeleza kwa ufanisi majukumu ya Bunge ya kutunga sheria, usimamizi na uwakilishi,” alisema.

Habari Zifananazo

4 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button