EAC yatumia akili bandia changamoto za muhogo

TANZANIA ni miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zilizofaidika na teknolojia ya akili bandia katika kutambua magonjwa ya zao la muhogo kwa kuangalia dalili zinazoonekana katika majani.

Katika mazungumzo na HabariLEO Afrika Mashariki jana, Mtafiti kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Kilimo cha Kitropiki (IITA), Neema Mbilinyi, alizitaja nchi nyingine za EAC zinazonufaika na teknolojia hiyo kuwa ni Kenya, Uganda na Rwanda.

Kwa Tanzania, Mbilinyi alisema teknolojia hiyo inatumika zaidi katika mikoa ya Geita, Mwanza na Kasulu mkoani Kigoma na Mkuranga katika Mkoa wa Pwani.

Mkuu wa Idara ya Uchechemuzi na Uratibu wa Rasilimali wa IITA, Dk Regina Kapinga alisema kituo hicho kinashiriki kongamano hilo kwa njia mbalimbali ikiwamo maonesho ya utafiti wa mazao kama muhogo na ndizi.

Awali katika mazungumzo hayo kwenye maonesho ya mazao yaliyofanyika katika viwanja vya IITA ikiwa ni sehemu ya programu za kongamano kubwa la chakula linaloanza leo Dar es Salaam, Mbilinyi alizitaja nchi nyingine nje ya EAC kuwa ni Mexico na Brazil.

Alisema teknolojia hiyo inayotumia simu ya mkononi ya akili bandia iitwayo Nuru, ina uwezo wa kutatua changamoto zinazotokana na magonjwa yanayoathiri mazao na kutoa elimu juu ya utambuzi na udhibiti wake.

“Nuru ni akili bandia katika utambuzi wa magonjwa na wadudu wanaoshambulia mazao, ina uwezo wa kutambua uwepo wa magonjwa kwa kuangalia dalili zinazoonekana katika majani,” alisema Mbilinyi.

Kwa mujibu wake, teknolojia hiyo pia ina uwezo wa kutambua magonjwa ya michirizi ya kahawa, batobato na athari za tanabui katika muhogo pamoja na athari zinazoletwa na viwavijeshi vamizi katika mahindi.

Alisema akili bandia hiyo inachunguza dalili zinazoonekana kwenye majani za ugonjwa na kwamba ikishatambua, humshauri mkulima namna ya kudhibiti magonjwa iliyotambua.

“Inaweza pia kumwelekeza mkulima wapi mahali anapoweza kupata mbegu bora, safi na salama zilizothibitishwa na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (Tosci),” alisema.

Aliongeza: “Faida nyingine ya teknolojia hiyo ni kufanya uchunguzi na kutoa matokeo papo kwa papo, kutoa ushauri wa namna ya kuyadhibiti magonjwa iliyoyatambua na inaweza kumuunganisha mkulima na wataalamu wa kilimo na watumiaji wengine waliopo maeneo ya jirani,” alisema.

“Inatumika kwa lugha mbalimbali ikiwemo Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa,” alisema na kuongeza kuwa hadi sasa zaidi ya wakulima na maofisa ugani 2,000 wanatumia teknolojia hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button