NAIROBI, Kenya: BARAZA la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika (EAPP Council of Ministers-COM) limekubaliana kwa pamoja kuwa na usimamizi madhubuti wa miradi mbalimbali ya umeme katika nchi wanachama, ili iweze kukamilika kwa wakati na kuwapatia wananchi nishati ya kutosha.
Kukamilika kwa miradi kutoka vyanzo mbalimbali vya umeme, kutawezesha nchi hizo kusaidiana pale nchi mojawapo inapokuwa na upungufu wa umeme huku msisitizo ukiwekwa kwenye miradi ya usafirishaji umeme.
(Transmission lines).
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko Februari 27, 2024 katika Mkutano wa 18 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika (EAPP Council of Ministers-COM) ambao unafanyika kwa siku mbili jijini Nairobi, Kenya.
“Baraza hili ni muhimu katika kuhakikisha nchi za Afrika zinaungana kwa ajili ya kuendeleza rasilimali za umeme zilizopo pamoja na kupata umeme wa uhakika kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na katika Mkutano huu kila nchi imeonesha utayari kufanya biashara ya umeme pale kunapokuwa na umeme wa ziada,” amesema Dk Biteko
Ameeleza kuwa kuna idadi kubwa ya watu katika nchi wanachama wa EAPP, hivyo inahitajika nishati zaidi kwa ajili ya maendeleo ya watu na viwanda na ndio maana kila nchi imejikita katika kuendeleza vyanzo mbalimbali vya umeme ajili ya kujipatia nishati ya uhakika.
Amesema kuwa, Tanzania itakuwa sehemu ya soko la umeme pale nchi jirani zitakapohitaji nishati hiyo, na hii ni baada ya kuwashwa kwa mashine zote Tisa katika Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere ambalo litazalisha megawati 2,115 ambazo zinatoa uhakika wa kutosheleza mahitaji ya ndani.
“Tanzania kuna njia mbalimbali za usafirishaji umeme (interconnectors) mfano Tanzania na Uganda, Tanzania na Burundi pamoja na Tanzania na Rwanda na sasa kuna laini ya umeme kutoka Tanzania hadi Kenya ambayo imekamilika na ipo kwenye majaribio itakayotuwezesha kufanya biashara kati ya nchi hizi mbili pale kila nchi ikiwa na umeme wa kutosha.” Amesema Dk Biteko
Ameongeza kuwa, kuna upembuzi yakinifu unafanyika chini ya Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kujenga mradi mkubwa wa usafirishaji umeme wa msongo wa Kilovoti 400 kutoka Tanzania hadi Uganda kutokea Shinyanga, ambao utasafirisha umeme mwingi zaidi kwa baadhi ya mikoa kama vile Kagera na pia kuwezesha nchi hizo kufanya biashara ya umeme.