Maajabu ya dunia, vitu vya asili vyamsukuma kuwa mwanajiolojia
JIOLOJIA ni sayansi ya asili inayojitolea kwa uchunguzi wa dunia na kusudi lake hasa ni kuelewa muundo wa mwili na muundo wa ndani na nje wa sayari, pamoja na michakato na mienendo tofauti. Jina lake linatokana na maneno ya Kigiriki Geo, “dunia” na logos, “maneno au ujuzi.”
Mtazamo wa wengi masuala ya sayansi huonekana kama mambo magumu lakini wako watu wengine sayansi kwao ni maisha wanayoyapenda, wanayoyaishi kwa maana ya kuyasomea na kuyafanyia kazi na moja ya sayansi hizo ni masuala ya jiolojia.
Leo nyota yetu imeangukia kwa Mwanajiolojia Vincent Edward anayefanya kazi na Kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania (PAET) baada ya kutaka kufahamu kwa nini aliacha fani zote akaamua kuchukua fani hiyo. Kazi ya kampuni ya PAET ni kuchunguza, kuchakata na kuzalisha gesi asilia.
Edward akiwa kama mwanajiolojia jukumu lake muhimu ni kuifahamisha kampuni inapopanga mipango ya uchunguzi na uchimbaji wa gesi.
Mwanajiolojia huyu ana miaka sita katika kampuni hiyo na alijiunga Mei 2017 kama mwanajiolojia baada ya kuhitimu Shahada ya Uzamili katika Jiolojia ya Petroli kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia nchini Norway.
Edward anasema kabla ya kuendelea na masomo zaidi aliwahi kufanya kazi katika sekta ya madini.
“Unajua jiolojia ni utafiti unaovutia wenye mambo mapya ya kujifunza na kugundua kila siku, nilitaka kuelewa kuhusu hewa ukaa, madini na maji vinavyotengenezwa na kuhifadhiwa katika ardhi,” anaeleza Edward kwa nini aliamua kuwa mwanajioloji.
Anaongeza kuwa alitamani sana kuchunguza mambo mbalimbali na aliamini kuwa mapenzi yake kwa vitu vya asili pia yalimsukuma kuwa na hamu na masuala ya jiolojia.
Edward anabainisha vitu vinavyomvutia kila siku katika jiolojia na kazi zake kama mwijiolojia kuwa ni maajabu mengi yaliyopo katika dunia.
“Unaweza kutumia jiolojia kufanya mambo mengi katika maisha yetu ya kila siku, kuanzia madini hadi nyenzo tunazotumia kujenga nyumba, hali kadhalika kupata nishati inayoendesha shughuli zetu…kinachovutia zaidi pia ni uwezo wa kuchunguza vitu ambavyo kwa kawaida huwa havionekani,” anaeleza Edward.
Kwa mujibu wa mwanajiolojia huyo kipengele cha jiolojia ambacho kinamvutia zaidi ni miundo ya kijiolojia na kuongeza kuwa hilo eneo la jiolojia linalohusisha umbo, mpangilio na muundo wa ndani wa miamba.
Lakini pia anasema anatamani kutafsiri picha za mtetemo ambazo ni pamoja na miundo inayotokana na mienendo ya dunia kwani husaidia kujenga picha kubwa na kuelewa vyema mienendo hiyo.
Akiwa kama mwanajiolojia ndani ya kampuni yake majukumu yake makuu ni kuandaa data ya kijiolojia na kuunda mifumo ya takwimu ya kijiolojia ambayo hutumiwa kama vigezo vya kuingiza hifadhi kwa ajili ya upangaji maeneo ya maendeleo kwa kampuni.
Edward pia hutayarisha ramani za mitandao za kijiolojia na mwonekano wa sehemu ili kuongoza shughuli mbalimbali ndani ya kampuni.
Mwanajiolojia huyo pia anahusika katika kupanga na kutambua maeneo yanayoweza kuchimbwa visima vipya, pamoja na kuandaa nyaraka zote za kijiolojia za uchimbaji wa awali ikiwa ni pamoja na mapendekezo ya kupata data ili kutoa msaada kwa Timu ya Operesheni katika kazi mbalimbali kama vile usimamizi wa uboreshaji na miradi ya ukarabati wa visima na uchimbaji.
Anasema pia jukumu lake lingine ni masuala ya uendeshaji kama vile kuunda na kuandaa ripoti za kila mwezi za uzalishaji wa gesi.
Edward anasema wakati anajiunga na PAET alianza kufanya kazi kama mwanajiolojia na majukumu yake yamebaki sawa ingawa wigo wa majukumu umeongezeka na kubadilika, jambo linamsukuma kujifunza kila siku ili kukabiliana na mabadiliko ya kimajukumu.
Akizungumzia PAET anasema ina jukumu muhimu katika maisha ya watu, kuanzia wafanyakazi wake, kizazi cha vijana (wanafunzi) na jamii kwa ujumla.
Edward anasena gesi inayozalishwa hutumika kuendesha asilimia kubwa ya uzalishaji wa umeme nchini Tanzania kwa njia safi, inayotegemewa na yenye bei nafuu zaidi na pia ikitumika kuendeleza viwanda vingi mkoani Dar es Salaam.
“Matokeo yake, bidhaa zao mara nyingi ni za ubora na za bei nafuu zaidi. Kila siku Watanzania hutumia bidhaa nyingi zinazotokana na uzalishaji wa gesi, kupata vifaa vya kupikia, vinywaji baridi na hata sabuni… kazi ya kampuni yetu inaweza isionekane kwa watumiaji, lakini ukweli tunahusika na maisha ya Watanzania, huenda kama huduma hii isingekuwepo huenda maisha yangekuwa magumu zaidi,” anasema.
Kwa mujibu wa Edward mbali na uzalishaji wa gesi, kampuni yao ni mwajiri bora ambaye anajali sana wafanyakazi wake na familia zao kwa kuhakikisha mazingira ya kazi ni salama na kuwasaidia kuendeleza familia zao kifedha.
Edward anasema vilevile kampuni hiyo imejikita katika kukuza ujuzi na inatoa fursa za ukuaji kwa wafanyakazi wake kupitia uwekezaji wa makusudi katika mafunzo na wanasaidia kizazi kipya cha Tanzania kwa kutoa fursa za mafunzo kwa vitendo, ufadhili wa matukio mbalimbali, msaada wa kiufundi, uelewa na kadhalika na inaandaa wataalamu wa siku zijazo.
Pamoja na yote hayo, Edward anasema kampuni yao pia ina jukumu chanya katika jamii kwa kutoa huduma bora za afya, vyumba vya madarasa na maji safi kwa jamii inayoizunguka.
“Mwisho kabisa naamini PAET ni walipakodi wazuri na wana mchango mkubwa katika kuisaidia serikali inapojitahidi kufanya maisha ya Watanzania wote kuwa bora zaidi,” anasema.
Kwake binafsi Edward anasema mwajiri wake amechangia katika ukuaji wa maisha yake kibinafsi na kitaaluma.
“Kampuni imenipa fursa ya kupata mafunzo ya kimataifa na uzoefu ambao umeniongezea ujuzi na kunisaidia kupata ujuzi mpya. Imenisaidia kujiboresha kila siku na pia nina fursa ya kufanya kazi kwa karibu na washauri wa kimataifa kwenye miradi mbalimbali, hasa mradi wa 3D seismic ambao nilihusika nao kuanzia hatua ya kubuni, usimamizi wa zabuni na awamu za utekelezaji,” anasema Edward.
Edward anasema mwajiri wake huyo amemjengea uwezo wa kitaaluma na kujiamini, imemtayarisha kusimamia na kuongoza miradi ya siku zijazo katika eneo lake la utaalamu.
Baada ya kazi kuna maisha mengine kama njia ya kupumzika, Edward anakubaliana na hilo na anasema muda wake wa mapumziko huutumia kufurahi na familia yake na marafiki.
“Ninapenda kuandaa nyama choma nyumbani na kuwaalika watu. Pia ninapenda kusafiri na kuvinjari maeneo mbalimbali ulimwenguni, haswa nikiwa na mke wangu na familia,” anabainisha mwanajiolojia huyo.
Edward anasema pia hufurahia vitu vya asili, kuogelea na kutazama televisheni, hasa soka na kutazama chaneli anayoipenda sana ya ‘Nat-Geo Wild’ kupitia king’amuzi cha DSTV.
Mwanajiolojia Edward anamaliza kwa kusema, “lakini jambo kubwa zaidi natumia muda kutafakari, kwani ni njia maalumu kwangu kuungana na muumbaji wangu.”