DAR ES SALAAM: Elimu ya Watoto Njiti imeingizwa kwenye mtaala mpya wa elimu na sasa litaanza kufundishwa katika shule za msingi.
Akizungumza leo Mei 03, 2024 kwa niaba ya wadau wa masuala ya afya ya uzazi, Mkurugenzi Mtendaji wa Taaasisi isiyo ya kiserikali ya Doris Mollel, Doris Mollel amesema elimu hiyo itafundishwa katika masomo ya Sayansi na Bailojia.
“Wazazi huko baadae watakaotoka mashuleni hawatakuwa na ile dhana kama iliyopo sasa kwa jamii, sio wale watakaosema mtoto huyu nimempata njiti kwa sababu mama yangu alikuwa hampendi mke wangu, au kuingiza imani za kishirikina, wengine wanawaza kutoboa watoto macho mambo mengi yanaendelea kwenye jamii yetu,”amesema |Doris
Aidha, amesema kama wadau wa masuala ya afya ya uzazi, wamefarijika serikali kuchukua hatua za kutoa muda wa kutosha kwa wanawake wanaojifungua watoto njiti, kwani harakati zao za kupambania sheria ya kazi na mahusiano kazini ya mwaka 2004 zimezaa matunda.
Isome pia https://habarileo.co.tz/ummy-atoa-neno-likizo-wanaojifungua-watoto-njiti/
“Tulianza harakati za kupambania mabadiliko ya sheria hiyo ya likizo ya uzazi tangu mwaka 2017, tunashukuru uamuzi wa serikali kutohesabu likizo ya uzazi kwa watakaojifungua Watoto Njiti utachangia kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa kiasi kikubwa.
“Tulikuwa na ombi la wakina baba ambao wake zao wanazaa watoto njiti wapewe mwezi mmoja wa mapumziko, lakini ombi hilo limegonga mwamba, ila tunashukuru na kupongeza hatua hii ya serikali kwa wakina mama wanaojifungua watoto njiti.
“Wakina mama ambao wanajifungua kabla ya wakati wanapitia changamoto nyingi sana, wengine wamepoteza kazi kutokana na kumuhudumia mtoto muda mrefu.”amesema
Amesema, katika harakati zao walikua na ajenda nne ambazo ni walizizindua mwaka 2021 ajenda ya kwanza likizo ya uzazi, serikali itenge bajeti ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, bima ya watoto njiti na elimu ya watoto njiti.
Isome pia https://habarileo.co.tz/wanaojifungua-watoto-njiti-kuongezewa-muda-wa-likizo/
“Bima za afya zimeshawatambua wazazi hawatoi tena fedha, serikali pia imetenga bajeti ya sh bilioni 23.36 kwa ajili ya watoto njiti, kununua vifaa tiba, kusomesha wauguzi na sasa imeondoa likizo kwa wanawake wanaozaa watoto njiti hii kwetu ni faraja kubwa,”amesema Mollel.
Aidha Mollel amewashukuru wadau mbali mbali waliofanikisha harakati hizo wakiwemo Wataalam wa Afya, Wazazi wa watoto njiti, Wataalam wa Sheria, Chama cha Madaktari wa Watoto Wachanga, Umoja wa Wake wa Viongozi, Mtandao wa Haki ya Afya ya Uzazi, Shirika la Kazi Duniani (ILO), Wadau wa Utatu ambao ni Chama cha Waajiri (ATE), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE).