Elimu ya choo bora yapigiwa debe
![](https://habarileo.co.tz/wp-content/uploads/2023/11/WhatsApp-Image-2023-11-24-at-3.53.17-PM-2-780x470.jpeg)
DAR ES SALAAM: ELIMU imetakiwa kutolewa zaidi ili kuelimisha na kuhamasisha watanzania kuwa na matumizi bora ya vyoo majumbani na maeneo ya huduma za kijamii.
Hayo yamesemwa leo Novemba 24, 2023 na Mkuu wa Idara ya Sera, Uraghabishi na Ushawishi kutoka Water Aid, Christina Mhando wakati akikabidhi vifaa vya usafi katika vituo viwili vya afya wilayani Temeke ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya siku ya choo duniani ambayo hufanyika Novemba 19 kila mwaka.
Vituo vilivyopatiwa msaada kupitia kampeni yao ya “Choo safi, Hadhi Yangu” ni kituo kipya cha Mkondogwa kilichopo Chamazi na Goroka klichopo Tuangoma.
Vifaa vya usafi vilivyotolewa ni pamoja na fagio, sabuni, vifaa vya kuhifadhia taka, mabuti, majaketi ang’avu na glavu ngumu.
Aidha, amesema suala la vyoo ni suala la msingi, takwimu za afya za mwaka 2022 (TDHS) zinaonyesha licha ya kuwa na ongezeko la vyoo bora kutoka asilimia 21 mwaka 2016 hadi asilimia 75 mwaka 2022 bado kuna changamoto kubwa kwa watanzania katika matumizi ya vyoo bora.
“Bado watanzania wanatakiwa kuhamasishwa ili kuwa na matumizi bora ya vyoo majumbani., Water Aid tunaamini kila mahali kila mtu awe na huduma hiyo, ikiwa nyumbani tumefanikiwa hata vituo vya kutolea huduma za kijamii husuani afya inapaswa kuwa hivyo,”amesema Christina na kuongeza
“Kuna tafiti mbali mbali zinaonyesha tupo vizuri lakini mara nyingi huduma hizo kufikika huwa ni ngumu, aidha matundu ya vyoo hayatoshelezi au vyoo vipo mbali hususani huduma za mama na mtoto, mama aliyetoka kujifungua analazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya choo ambayo inaondoa utu na hadhi yake,”amesema.
Water Aid, wameiomba serikali na wadau mbali mbali kuelekeza rasilimali kwenye vituo vya afya ili kila kituo kiwe na vyoo bora na maji ya kutosha ili kukidhi mahitaji ya wateja hususani pembezoni mwa mji.
Kwa upande wa Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke, Timoth Bende alishukuru msaada huo na kudai kuwa vituo hivyo ni vichanga, vitasaidi kuboresha na kuhimarisha usafi kwenye sehemu za kutolea huduma sana sana upande wa vyoo.
“Kama Manispaa ya Temeke tunawashukuru kwa kutambua kuwa tunauhitaji na kutoa kipaumbele na kuvifikia vituo viwili ambavyo ni vipya kabisa, mfano kituo cha Mkondogwa kilichopo Chamazi kinahudumia kata nyingi zenye wakazi zaidi ya laki mbili,”amesema.