‘Elimu ya kodi imenisaidia kutambua vishoka TRA’

MFANYABIASHARA wa madini katika machimbo ya Matabi, Wilaya ya Chato mkoani Geita, Marik Ngutti amesema elimu ya kodi imemsaidia kuwatambua vishoka wanaojitambulisha kuwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Ngutti ametoa ushuhuda huo katika Banda la TRA katika maonesho ya Wakandarasi, Wahandisi na Sekta ya Ujenzi Tanzania yanayofanyika katika Viwanja vya EPZA Bombambili Halmashauri ya Mji wa Geita.
Ameema akiwa katika maeneo ya migodi alikuta watu hao wakiwatoza wafanyabiashara kodi kwa kuwakadiria kiasi cha kulipa na walikuwa hawatoi risiti, hivyo akawa anawajulisha kuwa hao sio wafanyakazi wa TRA kwa kuwapa namba za kupiga Makao Makuu.
“Niliwaangalia sikuona utambulisho wao na pia walikuwa hawatoi risiti. Nikawaambia wafanyabiashara hawa siyo watu wa TRA bali ni matapeli,” amesema.
Isome pia:https://habarileo.co.tz/tra-yatoa-elimu-ya-mlipakodi-kahama/
Amesema wafanyabiashara wanatakiwa kuendelea kupewa elimu, ili wajiepushe na matapeli wanaohujumu serikali.
Naye Ofisa Mkuu msimamiz wa Kodi wa  TRA, Lutufyo Mtafya amesema wanashiriki kwenye maonesho hayo kwa ajili ya kufanya usajili na kuwasaidia wafanyabiashara namna ya kujisajili kupitia mfumo wa Tehama.
“Katika kipindi cha siku tatu tumetoa namba za usajili za mlipakodi 30 na kusambaza mashine za EFD na ndio ujumbe wetu mkubwa kusisitiza wananchi kudai risiti na wafanyabiashara kutoa risiti,” amesema Mtafya.
Mwenyekiti wa maonesho hayo George Mandia, amesema maonesho hayo yanatarajiwa kwa kiasi kikubwa kusaidia kuinua uchumi wa wakazi wa mkoa huo na kuwaunganisha wakandarasi, wahandisi na sekta ya ujenzi kwa ujumla Tanzania.

Maonesho hayo yalianza  Aprili 18 na yanatarajiwa kumalizika Aprili 28 na yamelenga zaidi kutoa elimu na kubadilishana ujuzi juu masuala ya ukandarasi na ujenzi. Kampuni zaidi ya 50 kutoka nchi mbalimbali duniani na wajasiriamali zaidi ya 100 wanashiriki maonesho hayo.

Habari Zifananazo

Back to top button