Elimu yahitajika mabadiliko tabianchi

NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Khamis Hamza Khamis amevitaka vyombo vya habari, taasisi na wadau wa mazingira kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa utunzaji na uhifadhi wa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza leo Mei 26, 2023 wakati wa hafla ya zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Buigiri, Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma, alisema suala la uhifadhi wa mazingira ni jambo mtambuka linalohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali.

Akifafanua alisema uhifadhi na utunzaji wa mazingira ni jambo muhimu kwani unabeba mustakabali wa viumbe hai, rasilimali na maliasili zilizopo nchini katika uso wa dunia.

“Mabadiliko ya tabianchi ni ongezeko la muda mrefu la joto la wastani la dunia na kusababisha kubadilika kwa mfumo mzima wa hali ya hewa, ili kuinusuru jamii yetu kutoka kwenye changamoto hizi tunapaswa kupanda miti kwa wingi ili kuokoa maisha ya viumbe hai wengine pamoja na binadamu” Alisema naibu waziri.

Aidha alisema serikali imeanza kampeni ya kupanda miti mashuleni ijulikanayo kama ‘SOMA NA MTI’ yenye lengo la kuhamasisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

“Lengo la kampeni hiyo ni kuwafanya wanafunzi waone zoezi la upandaji miti kuwa ni sehemu ya maisha yao ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame na uhaba wa maji,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button