Elimu yahitajika wajasiriamali kujisimamia wenyewe

OFISA Afya Mazingira Kata ya Viwandani jijini Dodoma, Gwantwa Mbwile amesema elimu bado inahitajika kwa wajasiriamali ili waweze kujisimamia wenyewe, waepukane na faini wanazotozwa kwa mujibu wa sheria ndogo za jiji.

Alisema hayo Jumapili wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye oparesheni ya ukaguzi wa usafi uliofanyika kwenye masoko ya Jiji la Dodoma na maeneo mengine.

Alisema elimu bado inahitajika kwa wajasiriamali ili waweze kujisimamia wenyewe, waepukane na faini wanazotozwa kwa mujibu wa sheria ndogo za Jiji.

Alisema elimu hiyo ikitolewa mara kwa mara kwa upande wao watakuwa kwenye mazingira mazuri kiafya kwa kuwa watapima afya na kuvaa sare na maeneo yao wanayofanyia kazi yatakuwa safi.

“Sisi kama maofisa afya wa Jiji la Dodoma tunahakikisha tunatoa elimu kwa mamalishe na babalishe kufuata sheria zote kama vile kuchemsha maji yao ya kunawa, kuvaa sare na kupima afya, kwa ajili ya kuwakwepesha wasilipe faini ya shilingi 50,000 hadi shilingi 300,000 au kuburuzwa mahakamani,” alisema.

Hata hivyo, amewataka wafanyabiashara wa soko la Sabasaba jijini Dodoma kuhakikisha suala la usafi linakuwa la kudumu kwenye maisha yao, badala ya kusubiri mpaka siku ya Jumamosi.

Kwa upande wake Ofisa Afya wa Jiji la Dodoma, Abdallah Mahia amewataka mamalishe na babalishe kufuata sheria zinazotolewa na Halmashauri ya Jiji ikiwa ni pamoja na kupima afya zao mara kwa mara na kuvaa sare wanapokuwa kazini.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button